Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SHIRIKISHO la Mpira wa kikapu hapa nchini (TPB) limeiomba Serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa ukumbi wa michezo (Arena) kama walivyoahidi ili kuleta mapinduzi makubwa zaidi ya shughuli za michezo na sanaa hapa nchini.
Februari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alikuwatana na wawekezaji wa sekta ya Michezo kutoka Misri wanaotarajia kujenga sehemu kubwa ya Michezo mbalimbali (Sports Arena) hapa Nchini.
Lakini pia mwezi uliopita katika uzinduzi wa Albamu ya Msanii Harmonize, Dkt. Mwakyembe aliweka wazi mpango wa Serikali wa kutaka kujenga ukumbi maalumu wa muziki utakaotumika pia kwa shughuli nyingine za michezo hapa jijini utakaokuwa na uwezo wa kuingiza zaidi ya watu elfu 40.
Kumbi hizo maalum hazitajengwa Dar es Salaam pekee bali hata katika
maeneo mengine ambayo wataona yanafaa kwa kushirikisha sekta binafsi.
Lakini ongezeko la Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia kiasi cha sh. bilioni 40.1 kutoka sh. Bilioni 30.9 kwa mwaka wa fedha uliopita kumewapa matumaini zaidi wadau mbalimbali wa michezo ambao wanatamani kuona mazingira ya miundombinu ya michezo ikiimarika zaidi.
Rais wa TBF, Phares Magesa ameliambia Majira kuwa, wao kama wadau wa michezo bado ombi lao kwa Serikali ni kutoa kipaumbele katika ujenzi wa Arena hiyo itakayochangia maendelea makubwa ya shughuli za michezo hapa nchini.
Amesema, tayari mara kadhaa walikuwa wakiomba Serikali kuboresha hali ya uwanja wa ndani wa Taifa ‘Indoor Stadium’ na viongozi mbalimbali wa Serikali walitoa ahadi ya kukarabati uwanja huo.
Lakini baada ya ahadi wa Waziri wamesema hawaoni tena haja ya ukarabati wa uwanja wa Ndani wa Taifa bali nguvu kubwa iwekezwe kwenye ujenzi wa Arena hiyo.
Magesa amesema kuwa, endapo Serikali itafanikiwa kujenga ukumbi huo mapema kama walivyoahidi basi ni wazi nchi itapata manufaa makubwa ikiwemo kupewa uwenyeji wa mashindano mbalimbali kama ilivyo kwa majirani zetu, Rwanda.
Toka nchi hiyo imejenga uwanja wa Kigali Arena wameweza kupata uwenyeji wa mashindano mbalimbali makubwa ikiwemo ya mchezo wa kikapu baada ya kuwewa uwenyeji wa mashindano ya Kikapu ya Afrika, nusu fainali na fainali za mashindano yanayosimamiwa na NBA , mashindano ya ya kikapu ya ‘Giants of Africa’ na mengine mengi.
“Tunaiomba na kuikumbusha Serikali kuweka na kutoa kipaumbele katika ujenzi wa Arena ambayo kwa kiasi kikubwa itachangia pia kukuza haraka shughuli za sanaa pamoja na michezo mingine, lakini pia uwepo wa uwanja huo utapelekea Tanzania kupata uwenyeji wa michuano mbalimbali mikubwa ambayo pia itachangia kuitangaza zaidi nchi yetu na vivutio vilivyomo, ” amesema Magesa.
Mbali na Serikali kutoa ahadi hiyo, lakini pia wadau mbalimbali wa michezo kutoka katika mashirika na watu binafsi wanapaswa kuwekeza nguvu zao katika ujenzi wa miundombinu ya michezo ili kuweza kuleta maendeleo zaidi katika sekta hiyo.
Aidha Magesa amewataka wachezaji wa kikapu kuendelea na mazoezi yao binafsi kwa kipindi hiki ili kulinda viwango vyao na kujikinga na ugonjwa wa Corona.
More Stories
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship
Mnzava apania kuwapeleka vijana Simba na Yanga