Na Mwandishi Maalum, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi wa mikoa ya Pemba kuwatoa hofu wananchi juu ya maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na badala yake waendelee kujikinga kama walivyopewa maelekezo na wataalamu wa afya.
Dkt.Shein aliyasema hayo jana katika Ikulu ndogo iliyopo Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipofanya mazungumzo na viongozi wa mikoa ya Pemba.
Katika maelezo yake Rais Dkt.Shein aliwasisitiza viongozi hao kuendelea na mikakati yao waliyoiweka kisiwani humo katika mapambano ya janga hilo na kuwataka kuendelea kuhakikisha wanatoa maelekezo kwa wananchi kama vile yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Alisema kuwa, viongozi hao wa mikoa yote ya Pemba wamefanya kazi kubwa na nzito hasa ikizingatiwa kuwa dunia imepata mtihani mkubwa wa janga la vizurisi hivyo vya corona na ndio maana WHO limetangaza kuwa hilo ni janga la Dunia.
Rais Dkt.Shein alieleza namna Serikali zote mbili zilivyolifanyia kazi suala la kupambana na maradhi ya virusi vya corona na kuongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake ilitoa taarifa zake yakiwemo mambo kumi pamoja na kutoa taarifa kwa kuwaeleleza wananchi juu ya ukweli wa janga hilo.
Alieleza, jinsi tahadhari zote zilizotolewa na Serikali kupitia wataalamu wake wa afya ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa kwa wananchi wote na kutoa pongezi kwa wananchi kisiwani humo kwa kuitikia wito huo.
Rais Dkt. Shein alisema kuwa, yeye na Rais John Pombe Magufuli hawakuwa tayari kuzuia wananchi kusafiri na kufanya shuhuli zao za kimaisha na badala yake waliwataka wananchi kuendelea kuelimishwa juu ya kujikinga na janga hilo.
Aidha, Rais Dkt.Shein alipongeza juhudi zilizochukuliwa na viongozi hao wa mikoa ya kisiwani Pemba na kusisitiza kuwa ni vyema juhudi zikaendelezwa katika kuwaelimisha watu hasa wale wa vijijini.
Alieleza kuwa, wapo baadhi ya watu ambao hawatoi ushauri mzuri kwa Serikali na wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii vibaya kuilazimisha Serikali jambo ambalo Serikali haiko tayari kulazimishwa katika kufanya wanavyotaka wao.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam