December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein

Rais Shein atoa wito kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wote kuzingatia miongozo inayoendelea kutolewa mara kwa mara na Wizara ya Afya ili kujiadhari na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Wito huo aliutoa jana kupitia risala yake ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka 1441 Hijriya ambao ni sawa na mwaka 2020 Miladiya.

“Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataala. Tunamshukuru yeye kwa kuturuzuku neema ya uhai na kutuwezesha kuupokea na kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1441 Hijriyah, sawa na mwaka 2020 Miladiya.

“Kadhalika, tuna wajibu wa kumshukuru Mola wetu Mlezi kwa kutuwezesha kuendelea kuishi kwa salama na amani. Tukiwa tunaingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu, tunapaswa tuwakumbuke wenzetu tuliofunga nao pamoja katika Ramadhani iliyopita, ambao hatunao tena, kwani wameshatangulia mbele ya haki.

“Tunamuomba Mola wetu Mtukufu awasamehe makosa yao, na awalaze mahali pema peponi Inshallah. Sisi tulio nyuma yao, tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe umri mrefu na wenye kheri, afya njema, nguvu na uwezo zaidi wa kutekeleza maamrisho yake, ili tupate mafanikio ya duniani na akhera,”alifafanua Rais Shein

Pia Rais Shein alibainisha kuwa, tunaukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 2020, ikiwa tumekabiliwa na mtihani wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Alisema, maradhi hayo tangu yalipojulikana mwezi Disemba 2019, katika mji wa Wuhan katika Jamhuri ya Watu wa China, yamekuwa yakienea kwa kasi katika nchi mbalimbali yakiambatana na vifo vilivyozua hofu, taharuki na yameleta athari kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi nyingi.

“Shirika la Afya la Duniani (WHO) limeyatangaza maradhi hayo, kuwa ni janga la dunia. Maradhi haya ni katili sana na yanaweza kuyakatisha maisha ya mwanadamu mara moja, kama tunavyoelezwa na madaktari pamoja na wataalamu wa afya,”alibainisha.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Shein alisema, kesi ya mwanzo ya maambukizo hayo, iliripotiwa Machi 19,mwaka huu na taarifa ya mgonjwa huyo, ilitangazwa na Waziri wa Afya wa Zanzibar,Hamad Rashid Mohamed.

Pia Machi 22, mwaka huu,Rais Dkt.Shein alisema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alituhutubia Watanzania na alitutaka tufahamu kuwepo kwa maradhi hayo hatari nchini, ili tuchukue hatua zinazostahiki kwa lengo la kujikinga na kudhibiti maambukizo yake.

Vile vile, alifafanua juu ya mipango, dhamira na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuyalinda maisha ya Watanzania wote dhidi ya maradhi hayo.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Shein alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kulifanyia kazi suala hilo, Machi 19, mwaka huu ilimuagiza Waziri wa Afya wa Zanzibar,Hamad Rashid Mohamed atoe taarifa rasmi kwa wananchi ya kuwepo kwa maradhi hayo hapa Zanzibar na kuwaelezea wananchi hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuzichukua katika kuyadhibiti maradhi hayo.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitangaza mambo 10 yaliyopaswa yatekelezwe na Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi wenyewe.
Miongoni mwa mambo hayo, Rais Shein alisema ni pamoja na kupiga marufuku mikusanyiko ya aina zote ikiwemo mikutano, semina na kadhalika, na kuweka utaratibu wa namna ya kufanya shughuli nyingine za kijamii.

Pia kuzifunga skuli zote, madrasa, vyuo vya elimu ya juu na taasisi nyingine za elimu.

Kuwahimiza wananchi wote wachukue hatua mbalimbali za kiafya za kuzuia maambukizo ya COVID-19, kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi mbalimbali na wataalamu wa afya.

Pia kuzuia uingiaji nchini kwa watalii wanaokuja kwa kutumia ndege za kukodi pamoja na kuweka utaratibu kwa wananchi wanaorudi nchini.

Samba na kuyatekeleza mambo mengine mbalimbali yatakayopangwa na Serikali ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuukabili ugonjwa huu.

“Serikali ililazimika kufanya maamuzi hayo magumu yaliyokuwa na athari za kiuchumi na kijamii, kwa lengo la kuzilinda afya na hali za wananchi, ikiwa ndio msingi wa Sera ya Afya ya Mapinduzi ya Januari 1964, katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wote bila ya malipo na katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya 2015-2020.

“Katika jitihada za kupambana na maambukizo ya maradhi haya, kwa nyakati tafauti, viongozi mbalimbali wa Serikali, madaktari na wataalamu wa afya, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali wameendelea kuwaelimisha na kuwasihi wananchi kuhusu maradhi yanayosababishwa na COVID-19,”alisema.

Aidha, alisema katika jitihada zilizochukuliwa na Serikali, wananchi wameitikia wito wa viongozi mbalimbali na wamezingatia yale yote waliyoelimishwa na nasaha walizopewa katika kujikinga na maradhi hayo na kupunguza maambukizo yake.
Hata hivyo, Rais Shein alisema, bado elimu zaidi inahitajika, ili iwafikie wananchi wengi zaidi waliopo katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

“Serikali na wahusika mbalimbali inapanga kuongeza kiwango cha taaluma, ili wale ambao wanaonekana hawajazingatia vizuri elimu na taarifa zilizotolewa, nao waweze kuelimika zaidi.

“Tangu mgonjwa wa mwanzo alipothibitishwa na kutangazwa hapa Zanzibar, sote tumeshuhudia jinsi Wizara ya Afya iilivyokuwa ikitoa taarifa wakati wote kuhusu hali ya ugonjwa ulivyo pamoja na idadi ya watu walioathirika na maradhi haya.
Hadi tarehe 22 Aprili, 2020 jumla ya wagonjwa 83 wameripotiwa, kati yao watatu wamefariki na wanne wamepona na wameruhusiwa kurudi nyumbani. Kazi hiyo ya kutoa taarifa itaendelezwa na Wizara ya Afya kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa. Tunaendelea kumuomba Mola wetu ili, atulinde na atuhifadhi, kwa rehma zake, kutokana na maambukizo ya maradhi haya, ambapo kwa nchi za wenzetu idadi ya vifo pamoja na maambukizo ni kubwa.

“Nawanasihi wananchi wote wasizisikilize taarifa zisizo rasmi wanazozitoa watu wasiohusika, ambao hawana mamlaka ya kiserikali ya kutangaza taarifa za Serikali. Serikali yetu inafuatilia kwa karibu sana na kwa makini mwenendo wa maradhi haya nchini mwetu, na tukio lolote linalohusu ugonjwa huu hapa nchini na matukio mengine yatatolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wakati,”alifafanua.

Aidha, Rais Shein alisisitiza mambo matatu muhimu ambayo tunapaswa tuyazingatie na tutoe mchango wetu.

Kwanza, kuyafuata na kuyatekeleza maelekezo ya madaktari na wataalamu wa afya kutokana na yote yanayoelezwa kuhusu ugonjwa unaosababishwa na COVID-19.

Pili, tuyasikilize na tuyatii kwa ukamilifu maelekezo yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini na wengineo kwenye jamii.

Tatu, tuuendeleze utamaduni wetu uliojengeka miaka mingi kwa wananchi kuchangia huduma za jamii, ili lengo letu la kupambana na maradhi haya, liweze kufanikiwa.

“Kwa hivyo, ilivyokuwa janga hili ni tatizo letu sote, naamini kwamba wananchi mtakuwa tayari kuchangia juhudi za Serikali, katika Mfuko Maalum wa Kukabiliana na COVID 19, ulioanzishwa tarehe 4 Aprili, 2020.

“Mfuko huu utasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango na Akaunti mbili tayari zimeshafunguliwa kwenye Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), ambapo Namba yake ya Akaunti ni 0748946001 na ile ya benki ya CRDB ambayo ni 0150487185100 kama zilivyotangwa katika vyombo vya habari,”alifafanua Rais Shein.

Rais alisema,matarajio yake ni kwamba Wizara ya Fedha na Mipango itasimamia vizuri matumizi ya fedha hizo kwa mambo ambayo Serikali imeyabainisha na yatakayopangwa, yakiwemo kugharamia vituo vya karantini na utibabu wa maradhi ya COVID 19.

Pia kugharamia upatikanaji wa vifaa na nyenzo kwa ajili ya kuwakinga madaktari, wataalamu wa afya na wafanyakazi waliopo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya maradhi haya.

“Kusaidia gharama za ujenzi wa jengo la Maabara Mpya ya kisasa ya uchunguzi na utafiti wa virusi linalojengwa huko Binguni, Wilaya ya Kati Unguja, ili uchunguzi wa COVID 19 na virusi vingine ufanyike hapa Zanzibar badala ya kuzipeleka sampuli za wagonjwa huko Dar es Salaam.

“Kutoa motisha kwa madaktari, wataalamu wa afya, wauguzi na wafanyakazi wengine wa afya, walio mstari wa mbele kwenye mapambano haya.Kugharamia mambo mengine yoyote muhimu yatakayojitokeza katika kukabiliana na maradhi hayo. Tuzingatie kutoa ni moyo, si utajiri,îalisisitiza.

Wakati huo huo, Rais Shein alisema, tunaukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao umejaaliwa kuwa ni mwezi wenye neema, baraka na fadhila nyingi, na kwa vile Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla anatutakia yaliyo bora kwetu, ametuwajibishia tufunge siku zote zilizomo katika Mwezi huu Mtukufu.

“Katika Surat Al Baqara, kuanzia Aya ya 183 hadi Aya ya 187, Mwenyezi Mungu anatueleza wajibu wetu wa kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na namna ya kuitekeleza ibada hio. Kadhalika, anatufahamisha kwamba Yeye hatutakii waja wake mambo yaliyo mazito, na hivyo ameifanya ibada ya funga na nyinginezo ziwe nyepesi kwetu.

“Kwa mnasaba wa ibada ya saumu, Allah Subhanahu Wa Taala, anatuambia katika Aya ya 185 ya Surat Al Baqarah, sehemu ya mwisho ya aya hiyo yenye tafsiri inayosema:
ÖMwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na pia (anakutakieni) mtimize hisabu hiyo, na pia (anakutakieni) kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni, ili mpate kumshukuru.

“Kwa hivyo, nawanasihi waumini wenzangu nyote ambao mna uwezo wa kuitekeleza ibada hii ya saumu, muitekeleze ipasavyo kwa kufuata masharti yake aliyotuelekeza Mwenyezi Mungu Mtukufu, kupitia Kitabu chetu cha Quran na hadithi za Mtume wetu (SAW),”aliongeza Rais Shein.

Pia alisema, ili kupata miongozo zaidi ya kutekeleza ibada zetu kwa usahihi na umakini,ana uhakika kwamba mashekhe, maulamaa na viongozi mbalimbali wa dini, kama kawaida yao, watakuwa wakitoa mawaidha kwa namna ambavyo itafaa na itakuwa ya usalama, kulingana na hali inayotukabili nchini mwetu na duniani kote.

“Nawanasihi waumini tuutenge muda wetu wa kutosha, ili tuweze kuyakisikiliza mawaidha hayo katika redio na televisheni zetu. Hivi sasa teknolojia imekua, kwa hivyo tunaweza kusikiliza matangazo ya redio hata kupitia kwenye simu zetu za mkononi na kwa kufanya hivyo, tutajiepusha na mikusanyiko,”alisema Rais Shein.

Pia aliendelea kuwasisitiza kutoa zaka na sadaka na kusaidiana kwa namna mbalimbali, katika njia za halali zinazomridhisha Mwenyezi Mungu.