January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia:Tunapanga yetu, Mungu anatupangia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameongoza Watanzania kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni,Dkt. Faustine Ndungulile, huku akisema nafasi ya aliyekuwa amepata ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, itaelekezwa kwa Mtanzania mwingine mwenye sifa

Rais Samia alitoa kauli hiyo Desemba 2,2024 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa Dkt.Ndugulile ambaye anazikwa kesho.

Dkt. Ndungulile aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika alifariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India.

Rais Samia amesema; “Wanadamu tunapanga yetu, lakini Mungu anatupangia, Dkt. Ndugulile ameiweka nchi pazuri, lakini Mungu amechukua kilicho chake,”.

“Tutaingia tena kwenye mashindano tutatafuta Mtanzania mwenye sifa anayeweza kushindana na ulimwengu, tutaingia tena na tutaweka mtu mwenye sifa ileile kutuwakilisha,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema amepokea salamu nyingi za pole kutoka ndani na nje ya nchi, huku akiwashukuru viongozi waliofika kumuaga Dkt. Ndugulile hasa kutoka Shirika la Afrika Ulimwenguni (WHO).

“Mengi yamesemwa, na tumeyasikia mengi katika mchango wake kwa nchi na duniani, uongozi wake, mchango wake katika taaluma ya tiba na siasa hasa kwa wananchi wa Kigamboni,”amesema.


Rais Samia amesema wajibu wa nchi ni kuimarisha uwakilishi wa Tanzania ndani ya nchi na Afrika hasa katika Shirika la Afya Duniani.

“Katika kuimarisha ushiriki wetu ni adhima ya Serikali kuhakikisha sasa Watanzania wabobezi tunaweka kila aina ya nguvu watuwakilishe katika fani za kimataifa.

“Dkt. Ndugulile alikuwa mwanajumuiya kutokana na imani yake ndicho kilichomsukuma akagombee nafasi hiyo na Serikali ikamuunga mkono tukajaliwa kupata nafasi ile, mwanadamu hupati unachokipata unapata majaliwa,”amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti, amesema Dkt. Ndugulile alikuwa na maono ya kufanya mageuzi katika shirika hilo.

Amesema tangu aliposhinda nafasi yake Agosti 2024, alishaanza kuandaa namna atakavyoliongoza Bara la Afrika katika nafasi yake mpya.

Amesema kupitia nafasi yake, tayari alianza kuandaa mambo kadhaa kwa kushirikiana na ofisi yake.


“Alitutembelea mwezi uliopita na alizungumza nasi mambo mengi kuhusu kile atakachokuja kukifanya na mageuzi anayoyataka.

Tulijiandaa kufanya vizuri zaidi katika uongozi wake na wengi walijiandaa wakiwemo wafanyakazi na wengine ambao tumekuwa tukifanya nao kazi,” amesema Dkt.