September 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia wataka wananchi kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Katavi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuacha kuvunja sheria kwa kuvamia maeneo ya hifadhi na badala yake watunze mazingira hayo.

Kauli hiyo imekuja kutokana na maombi ya Mbunge wa Mlele, Isack Kamwelwe aliyeomba kumegewa ardhi katika maeneo ya hifadhi ya mapori yaliyopo jimboni kwake.

Ameyasema hayo Julai 13,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi katika Wilaya ya Mlele, Kata ya Inyonga mkoani Katavi.

“Tunajua kuna uhaba wa ardhi na kuna maeneo ya hifadhi mnayatamani lakini hayaendani na kuvunja sheria tukae tuzungumze tuangalie namna ya kuyamega na si kuvamia,”amesisitiza Rais Samia.

Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu ombi la Kamwelwe la kuongezewa hekta elfu 15 katika Pori la Akiba Inyonga,Waziri wa Maliasili na Utalii,Angellah Kairuki amesema kuwa Wizara hiyo imepokea maombi hayo na inaendelea kufanya tathimini kuangalia uhitaji halisi na kuyawasilisha kwa mamlaka kwa hatua zaidi.

Amefafanua kuwa mwaka 2021 uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulitoka ambapo hekta elfu kumi zilipunguzwa kwa ajili ya wananchi wa Kijiji cha Kamsisi.

Katika hatua nyingine Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Inyonga kuendelea kushirikiana na Serikali katika utunzaji wa mazingira, misitu na kuhakikisha hakuna uvamizi katika mapori.

Pia amewapongeza wananchi wa Katavi kwa kuwa na jitihada katika shughuli za ufugaji nyuki ambapo kuna wafugaji zaidi ya 2132 ambao wamewezesha kupatikana kwa zaidi ya shilingi bilioni 21.5.