Na Iddy Lugendo, Timesmajira online
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Dodoma itaendelea kubaki kuwa Mji wa Serikali kama walivyotaka waanzilishi wa Nchi na viongozi waliopita katika Urais.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 25, 2022 alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa yaliyofanyika jijini Dodoma akisema kuwa hakuna kurudi nyuma.
Rais Samia amesema ataendelea kuenzi mawazo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na uamuzi wa Hayati Dk John Magufuli wa kuhamishia Serikali mkoani Dodoma na yeye hawezi kubadilisha chochote.
“Waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, Leo tunawakumbuka viongozi na waasisi wa nchi yetu ambao wao walianzisha na wengine walioendeleza amani, na misingi ya haki na utawala bora. Kwa kutambua heshima kuwa waliyoifanya viongozi hao hatuna budi kuendeleza yote waliyoyaasisi,” amesema Rais Samia.
“Ni katika viwanja hivi ambapo mwaka 2016, Hayati Dkt. John Magufuli alitangaza rasmi uamuzi wa kishujaa wa kuhamia Dodoma, Napenda kuchukua Fursa hii kusisitiza kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza uamuzi ule kama njia ya kutambua na kuenzi aliyoyataka baba wa taifa,” ameongeza.
Rais Samia amerudia kauli aliyoisema Hayati Dkt. John Magufuli kwa kusema kuwa “Makao makuu ya taifa hili la Tanzania ni Hapa jijini Dodoma na hakuna kurudi nyuma.”
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari