*Wasisitiza kuimarisha ushirikiano, Samia akaribisha sekta binafsi China kuwekeza
nchini, Jinping asema Tanzania mfano mzuri wa mahusiano kati ya nchi zinazoendelea
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, China
RAIS Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping katika ukumbi wa The Great Hall of the People ambapo pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa sekta binafsi chini China kuwekeza Tanzania katika uzalishaji wa vyanzo vya nishati mbadala na miundombinu ya usambazaji.
Aidha, katika mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia amesema uhusiano wa nchi hizo mbili ni muhimu na ametoa wito wa kuendelea kudumisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali pamoja na kuendeleza ushirikiano katika Maeneo ya Kuendeleza Miundombinu na Kukuza Uwekezaji (Belt and Road Initiative) ili kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.
Katika mutano huo, Rais Xi alisema kuwa China iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati yake na Tanzania ili kuleta manufaa zaidi kwa nchi zote mbili na kuendeleza uhusiano wa kihistoria ulioasisia na waasisi na kurithiwa na vizazi vya sasa.
Rais Xi pia alisema China inaiona Tanzania kuwa ni mfano mzuri wa mahusiano kati ya nchi zinazoendelea katika muktadha wa ushirikiano wa China na nchi za Afrika.
China na Tanzania zimekubaliana kuendelea kubadilishana uzoefu na kupeana mafunzo katika maeneo mbalimbali ya kiserikali.
Akizungumzia kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), Rais Samia ameeleza imani yake kuwa mkutano huo utakuwa na mchango mpya katika kuimarisha ushirikiano wa kirafiki kati ya Afrika na China na kuhamasisha mchakato wa viwanda na kilimo cha kisasa barani Afrika.
Baada ya mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia, Rais Xi Jinping na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema walishuhudia uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MOU) baina ya Tanzania, Zambia na China kuhusu uboreshaji wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Watu wa China (CPPCC), Mhe. Wang Huning.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato