December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia na safari mpya ya kukuza kilimo

Na Penina Malundo, Timesmajira Online

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa wakuu ni miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali 34 za Bara la Afrika waliohudhuria Mkutano wa Pili wa Kilimo na Chakula Barani Afrika.

Mkutano huo ulifanyika Dakar nchini Senegal kati ya Januari 25 – 27.

Mbali na wakuu wa nchi, mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri wenye dhamana ya kilimo na fedha, magavana wa Benki Kuu, viongozi wa jumuiya za kikanda (AU, SADC, ECOWAS, COMESA, EAC), wabia wa maendeleo, wakuu wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa taasisi za sekta binafsi, wataalam wa kilimo kutoka sekta ya umma na binafsi na wadau wengine wa sekta za kilimo.

Kupitia makala haya, Mwandishi wetu anaeleza miongoni mwa shughuli zilizofanywa na Rais Samia na fursa ambayo nchi ilipata na ambazo itanufaika nazo katika safari mpya aliyoanzisha kiongozi huyo mkuu wa nchi katika mikakati yake ya kukuza kilimo.

Mkutano huo uliandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na nchi mwenyeji – Senegal chini ya Uongozi wa Rais wa nchi hiyo, Macky Sall. Kaulimbiu ya Mkutano huo ilikuwa ni Kuilisha Afrika: Kujitegemea na Uhimilifu katika Uzalishaji wa Chakula.

Akiwa kwenye mkutano huo, Samia alishiriki katika jopo la wakuu wa nchi na Serikali kueleza masuala mbalimbali muhimu kwa ajili ya kuleta mageuzi katika kilimo nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Kupitia jopo hilo, Rais alielezea umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika kilimo kwa kutatua changamoto za upatikanaji wa ardhi, mitaji, teknolojia na upatikanaji wa masoko.

Akisisitiza suala hilo, Rais alieleza kuwa kundi la vijana ni kubwa kwa kutoa mfano kwa Tanzania kuwa ni asilimia 34.5 ya idadi ya Watanzania milioni 61.7 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Aidha, alieleza Dira ya Kilimo ya Tanzania ya Ajenda 10/30 inayolenga kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Kupitia Ajenda 10/30 Serikali imeanzisha Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) ambayo itawagawia vijana wa kiume na wanawake maeneo ya hadi ekari 10 kwa kila mtu yakijumuisha wawekezaji katika mashamba makubwa yenye ukubwa wa kati ya ekari 1,000 hadi 20,000.

Wawekezaji hao watawezesha vijana kutumia teknolojia bora na kununua mazao yatakayozalishwa kwenye mashamba ya vijana na kuongeza thamani.

Vile vile, Rais alieleza namna Serikali yake inavyoshirikiana na taasisi za fedha katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji, hatua iliyofanikisha kupunguza riba ya mikopo ya sekta ya kilimo kutoka asilimia 15 hadi 9.

Pamoja na mkutano huo, Rais aliongoza majadiliano katika mikutano ya wadau yenye lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

***Masuala muhimu yaliyojadiliwa

Mkutano ulijadili kwa msisitizo suala la hali ya ongezeko la bei za vyakula duniani kutokana na athari za UVIKO -19, mabadiliko ya tabianchi na vita ya Urusi na Ukraine vinaendelea kuathiri usalama wa chakula duniani endapo hatua thabiti za udhibiti hazitachukuliwa.

Ilielezwa kuwa Bara la Afrika lina fursa nyingi kwa ajili ya kuendeleza kilimo, ikiwemo ardhi inayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula kutosheleza mahitaji ya Afrika na ziada kuuzwa katika mataifa mengine duniani.

Asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani haijatumika na kwa upande wa Tanzania ni takriban asilimia 24 ya ardhi inayofaa kwa kilimo haijatumika.

Katika kufikia malengo hayo, unahitajika utashi wa kisiasa na utayari wa Serikali na sekta binafsi katika kutekeleza mipango, mikakati na programu za kuendeleza kilimo pamoja na kutoa rasilimali fedha.

Kutokana na majadiliano yaliyofanyika katika mkutano huo, iliazimiwa yafuatayo;

Kila nchi ikamilishe mpango wa uwekezaji katika kilimo katika vipaumbele vya taifa (Country Compact) uliojadiliwa na wabia wa maendeleo na sekta binafsi wakati wa Mkutano wa Pili wa Kilimo na Chakula nchini Senegal. Kwa upande wa Tanzania vipaumbele vya uwekezaji ni ngano, mafuta ya kula (alizeti), mazao ya bustani (parachichi); na ufugaji (nyama na maziwa).

Mbili, kila nchi kuanzisha Kitengo Maalum cha Rais kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuendeleza Kilimo katika vipaumbele vilivyokubaliwa.

Tatu, kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa kwa kuainisha muda wa utekelezaji, viashiria vya kupima mafanikio pamoja na kuwa na sera, sheria na vivutio vya uwekezaji katika kilimo.

Nne, Kuendelea kuratibu upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia mpango.

Tano, kuongeza bajeti ya taifa kwa ajili ya kuendeleza kilimo ili kufanikisha mpango ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Malabo lenye lengo la kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti katika kilimo.

Sita, Wadau wa maendeleo na taasisi za fedha za kimataifa walionesha utayari wa kutoa Dola za Marekani Bilioni 30 kwa ajili ya kugharamia mipango ya maendeleo ya kilimo kwa nchi za Afrika.

Tume ya Umoja wa Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika walielekezwa kufuatilia upatikanaji wa rasilimali fedha hizo.

***Mikutano ya Tanzania na wabia

Mkutano wa Kilimo na Chakula ulienda sambamba na mikutano ya kila nchi ya kujadili mipango ya kilimo na chakula.

Mkutano wa Tanzania ulifanyika Januari 25, 2023 ukiongozwa na Dkt. Samia na kuwashirikisha wabia wa maendeleo na sekta binafsi.

Akifungua mkutano huo, Rais alieleza kuwa dunia inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa chakula.

Changamoto hiyo inatokana na hali halisi ya ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi, majanga yaliyoikumba dunia ikiwemo ugonjwa wa UVIKO 19 na vita kati ya nchi ya Urusi na Ukraine.

Majanga hayo yamesababisha baadhi ya pembejeo za kilimo hususan mbolea kuzalishwa kwa kiwango kidogo na ongezeko la gharama za usafirishaji, hivyo kuathiri upatikanaji na uwezo wa wakulima kumudu gharama hizo.

Katika hatua nyingine, mfumko wa bei unaotokana na bei za vyakula umesababishwa na hatua za Tanzania kufungua masoko mapya ya mazao ya kilimo iliyovutia wanunuzi wengi wa mazao kutoka nchi Jirani na hivyo bei za vyakula kwa walaji wa kawaida kuonekana kuwa zimepanda.

Kaulimbiu ya mkutano huu ni kuhakikisha wanazalisha na kujitosheleza kuilisha Afrika ikiwa ni haki ya wananchi kuwa na uhakika wa chakula muda wote.

Rais aliendelea kueleza kuwa kilimo ni mhimili wa ustawi wa maisha ya wananchi wa Tanzania na kimekuwa kikikua kwa wastani wa asilimia 4 na kuchangia katika pato la taifa kwa wastani wa asilimia 26.9; asilimia 65 ya malighafi za viwanda, asilimia 30 ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 100.

Rais aliwajulisha wajumbe wa mkutano kuwa tumejiwekea lengo la kufikia ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Tumeanza kuchukua hatua za kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Dola za Marekani milioni 127.8 mwaka 2021/2022 hadi Dola za Marekani Milioni 414.7 mwaka 2022/2023, kuweka unafuu kwa wawekezaji na wafanyabiashara kupitia sera za kodi, udhibiti kuendelea kusimamia amani na usalama wa nchi na vivutio vya uwekezaji.

***Kikao cha Rais Samia na uongozi wa OCP GROUP

Katika hatua nyingine, Januari 25, 2023 Rais alikutana na Uongozi wa OCP Group. OCP Group ni Kampuni ya Kimataifa yenye Makau Makuu yake Casablanca nchini Morocco ikiwa ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa madini ya fosforasi na mbolea duniani.

Katika maneno ya ufunguzi wa kikao hicho, Rais alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikishiriki katika utekelezaji wa mifumo mbalimbali ya utoaji wa ruzuku.

Mfumo wa ruzuku ulioanza kutekelezwa mwaka 2022/2023 umefanyiwa maboresho mengi ikiwepo kuwa na mfumo wa kieletroniki wa usajili wa wakulima.

Matumizi ya mbolea bado ni madogo ikiwa ni wastani wa kilo 19 za mbolea kwa hekta ikilinganishwa na viwango vya kimataifa cha angalau kilo 50 kwa hekta.

Rais, alitambua na kupongeza mchango wa OCP tangu kuwepo kwake hapa nchini mwaka 2017 katika upimaji wa afya ya udongo na usambazaji na uuzaji wa mbolea.

*** Maombi ya Serikali kwa OCP
Moja, Kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha na kujitosheleza kwa mbolea kwa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha mbolea, chokaa mazao (agricultural lime) na jasi (gypsum) kwa ajili ya soko la Tanzania na nchi nyingine za SADC.

***Mkutano wa Rais Samia na uongozi wa YARA

YARA International ni kampuni ya mbolea kutoka nchi ya Norway. Katika Mkutano wake na uongozi wa kampuni hiyo, Rais alitambua mchango wa kampuni hiyo katika kuongeza tija ya kilimo kupitia mbolea ikiwemo wakulima wa zao la tumbaku wanaonufaika na mbolea za Yara.

Aidha, Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Programu ya BBT.

*** Maelezo kutoka uongozi wa YARA

Uongozi wa YARA ulisema upo tayari kuisaidia Serikali ya Tanzania kwa kuwezesha utekelezaji wa Programu ya BBT na Agenda 10/30 kupitia mfumo wa PPP.

Mfumo wa PPP katika kuendeleza sekta ya kilimo utatumika kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs).

Tanzania itakuwa nchi ya kwanza itakayonufaika na mpango wa kuboresha afya ya udongo unaotekelezwa na kampuni yao. Upimaji wa afya ya udongo utafanyika baada ya kufikia makubaliano yao na Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO).

Tatu, upatikanaji wa nishati ya uhakika hapa nchini utawawezesha kuanzisha kiwanda cha mbolea chenye uwezo wa tani 300,000.

***Mkutano wa Rais Samia na uongozi wa AGRA

Rais alikutana na Heilemariam Desalegn, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya AGRA Januari 26 ,, Dakar Senegal.

*** Kilichosemwa na ujumbe wa AGRA

Ilitolewa taarifa kuwa AGRF 2023 itafanyika jijini Dar es Salaam Septemba 5-9 Septemba, 2023.

***Taarifa ya Serikali kuhusu AGRF

Serikali iliwajulisha AGRA kuwa Tanzania iko tayari kuandaa mkutano wa AGRF kwa tarehe zilizopendekezwa na kukubali kufanyika uzinduzi tarehe 16 Machi, 2023.

Aidha, Rais aliwajulisha AGRA kuwa mkutano huo utakuwa ni moja ya fursa za kuhamasisha kilimo biashara kupitia Agenda 10/30;

Baadhi ya mafunzo yaliyopatikana kutokana na mkutano huo ni pamoja na Tanzania kuendelea kutekeleza mipango yake kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo kutafuta rasilimali fedha.