January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia na dhamira ya kuyakabili Mabadiliko Tabianchi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA ni kati ya nchi nyingi duniani zinazokabiriwa na changamoto ya janga la mabadiliko ya tabianchi, licha ya serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kuonesha dhamira ya dhati ya kukabiliana na hatari hiyo duniani.


Miongoni mwa juhudi zinazofanywa na Rais Samia mbali na mambo mengine, ni kitendo chake cha kushiriki katika Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika kuanzia Novemba 30, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.


Ajenda kubwa zilizojadiliwa humo na washiriki mbalimbali akiwepo Rais Samia mwenyewe ni namna ya kuifanya Dunia iwe mahali salama kwa kubadili mwelekeo na kuchochea hatua za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.


Mkutano huo umepangwa kumalizika Desemba 12, 2023, ukiendeleza kile kilichoanzishwa mwaka 2015 kwenye Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi ukilenga kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya uzalishaji wa hewa ya ukaa ili kulinda uhai na kipato.


Wakati Tanzania ikiwa miongoni mwa washiriki wake kabla ya Rais Samia kuamua kukatisha siku za kuwapo huko na kurejea nchini baada ya kutokea mafuriko katika Kijiji cha Katesh, wilayani Hanang’ mkoani Manyara na kusababisha vifo vya 63, serikali yake imeandaa Sera kuhusu masuala ambayo nchi inachangia kupunguza uzalishaji wa gesi joto kama nia ya mkutano huo wa COP28 ambao ni fursa kwa nchi kuieleza Dunia na mchango wake kama nchi.


Akihutubia mkutano huo, Rais Samia, ameyataka mataifa duniani kutambua kuwa suluhisho la uhakika la kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ni kutimiza ahadi za kutoa fedha na kuongeza kasi ya mikakati ya kukabiliana na janga hilo.


Rais Samia anasema ilitolewa ahadi ya dola za Kimarekani bilioni 100 kila mwaka, ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi katika mkutano wa Copenhagen na ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya kiasi hicho kuwa kidogo kuliko kilichohitajika.


Kwa upande mwingine, Rais Samia alisema mkutano wa Paris na Ufaransa iliazimiwa kudhibiti ongezeko la joto chini ya nyuzi joto 1.5, lakini hali ni kinyume kwani kasi ya ongezeko la joto kwa sasa duniani inatia wasiwasi.


Rais Samia pia anasema kushindwa kutimiza ahadi kunapunguza mshikamano na imani na kuleta matokeo mabaya kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, ambayo hupoteza kati ya asilimia 2 hadi 3 ya Pato la la Taifa (GDP) kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.


Bara la Afrika Tanzania ikiwemo linaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi katika uchumi na maisha ya watu, hivyo kuna haja ya kuwepo mfuko maalumu utakaosaidia kukabiliana na athari zinazotokea.


Hata ukiangalia suala la mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang’ sababu kubwa ni mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni matokeo mabaya yanayokwenda kuathiri uchumi wa wananchi moja kwa moja. Kuna wakati joto linakua kubwa kupitiliza unaochangiwa na ukame wa hali ya juu. Kama hiyo haitoshi, wakati mwingine maeneo hayo kupokea mvua kubwa kupitiliza na kusababisha madhara makubwa kama ilivyotokea Hanang’.


Hata hivyo tumeshuhudia serikali ikifanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo lililojitokeza kama vile kupeleka vikosi vya ulinzi na uokoaji, kugharamia mazishi ya waliopoteza maisha bila kusahau majeruhi kupata ofay a kutibiwa bure na serikali ya Rais Samia, kama njia ya kuwafuta machozi waathirika.


Serikali ya Rais Samia inaendelea kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuanzisha kusimamia sera na miradi kama ule wa nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira, kilimo cha umwagiliaji kama njia mojawapo ya utunzaji wa mazingira.


Haya ni mambo muhimu yanayosimamiwa vizuri na serikali, kwa lengo la kupunguza athari za changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kama ilivyokuwa dira ya mkutano wa COP28.


Akisisitiza kwenye mkutano huo, Rais Samia anasema nchi yake ina nia ya kuhamasisha kuongezwa matumizi ya nishati safi ya kupikia na gharama nafuu ya teknolojia barani Afrika kwa lengo jema la kumkwamua mwanamke.


Naye Profesa Pius Yanda wa Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema nchi zilizoendelea zinahitaji kutoa fedha kutokana na uchafuzi wa mazingira zinazoendelea kuufanya kila siku.


“Nchi za Afrika ndizo zinazoathirika zaidi, licha ya mchango wake kuwa mdogo kwenye uchafuzi kutokana na mapinduzi ya viwanda duniani na kusababisha ukame, mafuriko vinavyohitaji kufidiwa na nchi zilizoendelea.


“Nchi hizo zinakiri na ziliahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 100 sawa na Sh Trilioni 2.5 kila mwaka, lakini hazikufanya hivyo,” anasema Profesa Yanda.


Mwanamazingira, Paul Samuel anasema mafuriko yaliyoambatana na maporomko ya tope yaliyotokea wilayani Hanang, mkoani Manyara, ambayo yametokea katika kipindi ambacho mkutano wa COP28 unafanyika, yanatakiwa kuifumbua Dunia kuhusiana na ukubwa wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi.


Madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo ni vifo vya watu 65, uhalibifu wa mali zikiwemo nyumba pamoja na madhara mengine yanayoigusa jamii moja kwa moja.


Katika kipindi hiki ambacho Hanang kumetokea mafuriko na maafa makubwa, ni fursa nzuri kwa washiriki wa mkutano huo kujitathmini kama njia za kukabiliana na makali ya tabianchi.


“Kwa hiyo ni muhimu washiriki wa mkutano huo wakatumia mfano wa kilichotokea Hanang ajenda muhimu, iwe fedha za kukabiliana na mabadiliko hayo,”Alisema.


Kufanikiwa kwa ajenda hiyo, kutaweka urahisi kwa Tanzania na nchi nyingine kufikia malengo, kama yalivyowekwa kwenye maazimio ya pamoja ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi,” anasema Samuel.


Anasema nchi tajiri lazima zitoe fedha kwa kuzingatia athari kubwa zilizosababishwa nchi na fedha hizo ziwezeshe nchi za Afrika Tanzania ikiwemo katika urekebishaji unaohitajika na kugharimia mahitaji yote ya hasara na uharibifu unaojitokeza.


“Tunatakiwa kutumia jukwaa hili (COP28) muhimu kujadiliana na kuingia makubaliano yenye manufaa kwa pande mbili, tukitambua hakuna mtu atakayeleta pesa bure bila yeye kunufaika,” anasema Samuel.


Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa sasa dalili za wazi na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi zinazoongezeka kote duniani.


Athari hizi zinatokea kwa kila nchi na hakuna aliye na kinga dhidi ya zahma hii na hakuna kisingizio cha kukwepa kuchukua hatua.


Kwa kutambua ukweli huu, ndiyo maana Rais Samia moja ya agenda zake kuu ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapa nchini, vinginevyo nchi yetu haitakuwa salama.


Ni dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatishia miongo ya hatua za maendeleo na kuweka hatarini mipango yetu yote ya maendeleo endelevu jumuishi.


Uamuzi wa Rais Samia, kutilia mkazo kukabiliana na mabadilkiko ya tabianchi kunatoa fursa ya kuongeza kasi ya maendeleo endelevu kupitia kuwa na hewa safi, kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya za wananchi na itatoa usalama na ukuaji wa uchumi kwa mataifa yote.


Bila kuunga mkono juhudi za Rais Samia maeneo mengi nchini, yatakumbwa na mafuriko na kusababisha watu kupoteza maisha na pia maelfu kukosa makazi kama ambacho tunakiona Hanang.


“Tunahitaji tufanye kazi bega kwa bega na sekta binafsi na asasi za kiraia, mabadiliko ya tabianchi duniani yanatuma ujumbe wa wazi, ndiyo maana Rais Samia ameupa kipaumbele mkutano wa COP28,” anasema mwanaharaka Egdar John.


Akisisitiza wajibu wa kila mmoja katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mwanaharakati huyo anasema;
“Sote tunaweza kupunguza mchango wetu wa hewa ukaa kila siku katika vyakula tunavyotumia, nguo tunazovaa, usafiri tunaochagua na taka tunazozalisha.


Kwa hakika tunahitaji kubadilisha mfumo wa matumizi yetu , hii sio tu dunia iliyopungukiwa bali pia ya matumizi ya kupindukia. Na ukweli unaoumiza ni kwamba tani milioni 1300 za chakula hupoteza bure kila mwaka ili hali watu takrinban milioni 2000 wanakabiliwa na njaa na utapiamlo.


Nayo ripoti mpya ya shirika la utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) inasema majanga ya asili, ikiwemo mafuriko, vimbunga, joto la kupindukia, kuongezeka kwa kina cha bahari na matukio kama el-nino vyote ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi.


Shirika hilo linatahadharisha mambo kuwa magumu zaidi endapo Dunia haitafanyia kazi juhudi na mbinu za kupunguza vitu vinavyochochea mabadiliko tabianchi.