July 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: Madeni vyombo vya habari yalipwe ifikapo Desemba

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameagiza Wizara na Taasisi za Umma zote zinazodaiwa na vyombo vya habari ifikapo Desemba, mwka huu ziwe zimelipa madeni hayo ili vyombo hivyo viweze kulipa mishahara wafanyakazi wao.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo jana jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini na Kikao Kazi cha Maafisa Habari wa Serikali kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Vyombo vya habari nchini vinadai wizara na taasisi za Serikali zaidi ya sh. bilioni 11, ambapo kwa uamuzi wake wa kuweka ukomo wa kulipwa kwa madeni hayo kutasaidia kutatua changamoto zinazokabili vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla.

Pamoja na agizo hilo, Rais Samia alivishukuru vyombo vya habari nchini kwa jinsi vinavyoshirikiana na serikali katika kutoa habari kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea katika jamii ikiwemo harakati za maendeleo na hata majanga yanapotokea

“Kama mlivyofanya katika maafa ya Hanag na wakati wa mvua za El nino zilizoisha hivi karibuni zilizoleta mafuriko huko Rufiji na maeneo mengine nchini “

“Pia kupitia kalamu na sauti zenu umma ulitambua na kuelewa hatari iliyokuwa mbele yetu na kuchukua tahadhari stahiki pia juhudi za uokozi zilifanyika kwa haraka sana na kwa ueledi, vilevile tulipata michango mingi kwenye Sekta ya wafanyabiashara na kwingineko,” alisema.

Alitaka vyombo vya habari kuendelea kutumia uhuru wao kwa weledi na kwa kuzingatia dhana ya uandishi wa habari wenye uwajibikaji.

Rais Samia alisema Serikali haina budi kuweka mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi katika kuimarisha uhuru na mazingira ya kazi ya vyombo vya habari.

“Serikali tutafanya yetu, lakini nanyi chezeni upande wetu,” alisisitiza. Mbali na hayo, Rais Samia alisema ulimwenguni vyombo vya habari vinarasimisha maudhui ambayo katika maeneo mengine yanakua ni tishio kwa mila na desturi na hali za kisiasa kwenye maeneo nchini, hivyo alivitaka vyombo hivyo kutimiza wajibu wake.

Katika hatua nyingine Rais Samia alipokea Ripoti ya Kamati Maalum kuhusu Kutathmini hali ya Utendaji na Uchumi kwenye Vyombo vya Habari Tanzania Bara ambapo amesema hali za kiuchumi kwa wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari hairidhishi huku wao wakiwa wasemaji wa mambo ya wengine.

Rais Samia pia alisema kuwa mabadiliko ya teknolojia yasiwe chanzo cha uharibifu wa taaluma ya habari kutokana na watu kufanya kazi kwa mihemko na presha ya mitandao.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alisema kuwa hali ya uzalendo kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini imeongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma.