January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia inatarajia kuzindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na mitaala iliyoboreshwa ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo.

Akizungumza jana jijini hapa na waandishi wa habari ,Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema uzinduzi huo utafanyika Januari 31 mwaka huu jijini Dodoma katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Prof. Mkenda alisema uzinduzi huu ni hatua muhimu katika kuboresha sekta ya elimu nchini na ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais aliyoitoa alipohutubia Bunge.

Prof. Mkenda amefafanua kuwa mchakato wa kupitia na kurekebisha sera hiyo umechukua miaka mitatu na tayari umekamilika.

Ameeleza kuwa marekebisho hayo yameidhinishwa na Rais kupitia Baraza la Mawaziri, huku mitaala mipya ikiwa imefanyiwa marekebisho makubwa kwa lengo la kuendana na mahitaji ya kisasa.

Alisema Mageuzi haya ya sera ni makubwa na yanatekelezwa kwa awamu, yakianzia na elimu ya awali na hatimaye kugusa vizazi vyote na Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya elimu nchini.

Mbali na uzinduzi wa sera hiyo na mitaala mipya, kutakuwa pia na maonyesho maalum ya masuala ya elimu huku akitoa wito kwa wadau wa elimu na wananchi kuhudhuria uzinduzi huo ikiwa ni hatua kubwa katika mabadiliko ya elimu nchini, na ni ishara ya dhamira ya serikali kuboresha maisha ya Watanzania kupitia elimu bora.