December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuzidi kutoa fedha kuimarisha majengo ya utawala

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha majengo ya utawala kwenye halmashauri zote nchini ikiwemo na ya wilaya ya Nyang’hwale.

Amesema ujenzi wa majengo hayo ya kutolea huduma kwa wananchi ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 ambayo imeielekeza Serikali kujenga miundombinu hiyo muhimu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nyangh’hwale ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 na umegharimu sh bilioni 3.7.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha majengo ya utawala kwenye halmashauri zetu lengo likiwa ni kuona wananchi wanapata huduma karibu na maeneo yao,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Idara na watumishi wote waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa katika kuwahudumia wananchi “Wananchi wana matumaini makubwa na Serikali yao, wahudumieni na mtatue kero zao.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni amesema mradi huo utakapokamilika utaboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wa halmashauri hiyo na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi kwenda katika halmashauri yao kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali zikiwemo na za kumalizia ujenzi wa jengo hilo ulioanza 2017/2018.

Baada ya kuweka jiwe na msingi la jengo la halmashauri, pia Waziri Mkuu amezindua jengo la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo litawawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya biashara na ujasiriamali.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo hilo ambalo limejengwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa aliwataka wakazi wa eneo hilo kutumia fursa kituo hicho kwa ajili ya kupata elimu ya biashara na ujasiriamali pamoja na mikopo ili wajiendeleze kiuchumi.

Aidha, Majaliwa amewataka wananchi hao kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Serikali. “Vikundi vinakopesheka kwa urahisi hata anuani yake ni rahisi”.

Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande ameipongeza Serikali kwa ujenzi wa kituo hicho kwani kitatoa fursa ya wafanyabiashara na wajasiriamali kupata elimu sahihi ya mikopo na kujiepusha na mikopo umiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga ameahidi kuendelea kusimamia ujenzi na uendelezaji wa vituo hivyo katika maeneo mengine nchini ili viweze kuleta tija kwa wananchi.

Awali, Mkuu wa wilaya hiyo, Grace Kingalame amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuidhinisha utoaji wa fedha ambapo katika wilaya yao wamepokea zaidi ya sh bilioni 25 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema kati ya fedha hizo shilingi tisa zimetumika katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini na tayari vijiji vyote vya wilaya hiyo vimepata umeme, pia zaidi ya shilingi bilioni 6.8 zimepelekwa katika utekelezaji wa miradi ya maji.