November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuwakabidhi wavuvi zana za kisasa

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan,anatarajiwa kuwasili jijini Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku moja ya kukabidhi vifaa vya kisasa vya uvuvi wa samaki kwa wavuvi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Januari 26,2024 kuhusiana na ugeni huo,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CPA Amos Makalla,amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Samia kwa wingi atakapowasili mkoani humu.

Amesema atawasili Januari 29, mwaka huu, majira ya mchana katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa.

“Tunatarajia ugeni wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wa ziara ya kikazi ya siku moja,Januari 30,2024 asubuhi atakabidhi vifaa vya uvuvi kwa vikundi mbalimbali vy wavuvi vilivyopo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, hafla itakayofanyika katika Uwanja wa Nyamagana,”amesema CPA Makalla.

Amesema vikundi vitakavyonufaika na zana hizo viko Kanda ya Ziwa,vimesajiliwa na vinafanya shughuli za uvuvi katika mikoa ya Mwanza,Mara,Kagera,Geita na Simiyu, hivyo zana hizo za kisasa vitaviwezesha kufanya uvuvi wa tija na endelevu.

“Rais Dk.Samia amefanya kazi kubwa ya kihistoria mkoani Mwanza na Tanzania kwa ujumla na anastahili kupongezwa kwa kazi hiyo iliyotukuka,rai yangu wananchi wajitokeze kumlaki atakapowasili katika uwanja wa ndege pia waje kumsikiliza katika mkutano wake baada ya kukabidhi vifaa vya uvuvi,”amesema CPA Makalla.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema zana hizo zimetolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ziwasaidie wavuvi kuondokana na changamoto ya matumizi ya zana duni za uvuvi wa samaki zilizopitwa na wakati.