January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuunda tume mbili sakata la Wamasai

*Ni kuhusiana na masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro

*Moja kuchunguza suala zima la uhamaji kwa hiari, asisitiza ushirikishaji wananchi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Arusha

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ataunda tume mbili,ambapo moja itachunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro.

Tume nyingine itaangalia utekelezaji wa
zoezi zima la uhamiaji wa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Rais Dkt. Samia, amesema hayo Desemba 1,2024, Ikulu ndogo ya Arusha wakati akizungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi katika eneo la Ngorogoro.

Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.

Rais Dkt. Samia aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na jamii hiyo.

Vilevile,amesisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.

Aidha,Dkt.Samia,amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye Serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro.