December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuongoza kumbukizi ya Sokoine

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Arusha

RAIS Samia Suluhu Hassan, leo anatarajia kuwaongoza Watanzania katika kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Hayati Edward Sokoine.

Akizungumza na wanahabari mjini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maadhimisho hayo.

Mkuu wa mkoa amemtaja Hayati Sokoine kama mtu aliyekuwa muadilifu na mchapakazi, huku akiwataka Watanzania kumuenzi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwaenzi viongozi waadilifu na wachapakazi wa sasa wenye sifa na uchapakazi wa kufanana na hayati Sokoine.

Makonda amemtaja Hayati Sokoine kama mtumishi mahiri na mwenye ujasiri wa kusukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania bila kuogopa na kuhofia vikwazo mbalimbali.

Mkuu wa mkoa ametembelea makazi ya hayati Sokoine eneo la Enguiki Monduli, kukagua maandalizi ya shughuli ya kesho ya kumbukizi ya miaka 40 tangu kifo cha hayati waziri mkuu wa Tanzania Edward Moringe Sokoine.

Hayati Moringe alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu tarehe 13 Februari, 1977 hadi 7 Novemba 1980, tena tangu tarehe 24 Februari 1983 hadi kifo chake, alipofariki kufuatia ajali ya gari.

Uongozi wake unatajwa kuwa wa mfano kwa jinsi alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi huku akikemea ulaji rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.