January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kujenga kwa lami barabara kuu Mkoa Singida

Na Thomas Kiani, TimesmajiraOnline,Singida

SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ina mpango mkakati wa kuinua uchumi Mkoa wa Singida katika miaka miwili ya bajeti mwaka 2023/2024 na 2024/2025 kwa kuziwekea lami barabara kuu tano zinazounganisha mikoa ya Tabora, Mbeya na Dodoma.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Mwigulu amesema hayo mwishoni mwa wiki kwenye sherehe za wazazi zilizofanika kimkoa Sepuka Madukani, mkoani hapa na kuhudhuriwa na viongozi wa chama, Serikali na wanachi.

Amefafanua juu ya barabara hizo, Waziri Mwigulu, alisema Barabara ya Sabasaba Singida Mjini hadi Kizaga kupitia Sepuka na Ndago Kilomita 77.6 tayari Serikali ya Mama Samia imetoa fedha sh. bilioni 88.583 na tayari kampuni ya Henan kutoka china imepewa kazi ya ujenzi na kazi itaanza mwezi ujao.

Mwigulu ameendelea kusema barabara zingine ni kutoka Misughaa hadi Kwamtoro, nyingine ni kutoka Singida hadi Mgungira kilomita 89 na inategemea kujengwa hadi Tabora nyingine ni kutoka Sepuka-Mlandala hadi Shelui na ya mwisho ni kutoka Itigi hadi Mbeya.

Mwigulu amesema barabara zote hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha wananchi kupata huduma za usafiri, kusafirisha mazao ya kilimo mifugo na uvuvi, hivyo wananchi wanaenda na kasi anayotaka Rais Samia katika kujiletea maendeleo kupitia fursa zilizopo kwenye maeneo yao.

Mwigulu amesema Rais Samia halali usingizi, akitaka wananchi wake wapate maendeleo na Taifa na amejitahidi kwa miaka mitatu amesonga mbele kiuchumi katika Sekta zote muhimu na Tanzania sasa ni nchi kati ya mataifa 20 duniani yanayosonga mbele kwa kasi kubwa kiuchumi na barabara hizo ni za kimkakati zitawaletea wananchi wa Singida maendeleo makubwa niaka mitano ijayo.

Waziri Mwigulu ambaye pia ni Mbuge wa Jimbo la Iramba Magharibi, alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo.

Amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kuwapatia huduma zote muhimu za kijamii kwa ukaribu zaidi.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amesema jimbo lake ni safi na linamkubali Rais Samia na Serikali yake kwa kuleta maendeleo nchi nzima kwa kasi kubwa.

Katika sherehe hizo, Kingu aliwakabidhi majiko 230 ya gesi walimu 230 wa shule za msingi na sekondari katika tarafa ya Sepuka yenye thamani ya sh. milioni 11.5.

Aidha, ametoa pedi milioni kwa wanafunzi wa kike shule za Sekondari tarafa ya Sepuka, shuka kwa wagojwa wa zahanati na vituo vya afya tarafa ya Sepuka na mipira kwa timu za mpira.