November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuandika rekodi mkutano G20

*Aalikwa kushiriki utakaofanyika Brazil, atakuwa Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuhudhuria mkutano huo tangu mwaka 2009

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan amealikwa kushiriki mkutano wa viongozi wa G20 utakaofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil kuanzia Novemba 18 hadi 19, 2024.

Mkutano huo una kauli mbiu isemayo; ‘Kujenga ulimwengu wa haki na sayari endelevu’.

Mwaliko huo kwa Rais Samia umetolewa na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil.

Katika mkutano huo Rais Samia atakuwa ni Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20 na Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa G20 tangu kupanuka kwa kundi hilo kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, historia inaonesha kuwa Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa na Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete walishiriki mikutano ya G8 iliyofanyika mwaka 2005 na 2008 mtawalia.

Ushiriki huo wa Rais Samia katika mkutano wa viongozi wa G20 unaashiria kuongezeka kwa ushawishi na mwonekano wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Wakati huo huo Raiis Samia , amepongezwa na mataifa ya kundi la G20 kutokana na juhudi zake za kuimarisha utawala bora, kukuza demokrasia, na maendeleo endelevu nchini

Kwa jitihada hizo Tanzania imepongezwa na jumuiya za kimataifa, ikiwa ni ishara ya mafanikio makubwa katika uongozi Serikali ya Awamu ya Sita ambapo mchango wa Rais Samia katika kuendeleza amani, usalama, na ustawi wa kiuchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Kutokana na jitahada zake, Tanzania imealikwa kutashiriki katika Mkutano wa Viongozi wa G20, ambapo Rais Samia , atawakilisha taifa kwenye mkutano huo.

Katika kipindi chake toka ameingia madarakani, Rais Samia ameonesha mwelekeo wa kipekee wa kiutawala kwa kutekeleza mageuzi muhimu katika sekta mbalimbali.

Hii ni pamoja na kuhakikisha uwazi katika utendaji wa Serikali, kupambana na rushwa, na kuboresha hali ya haki za binadamu, hasa haki za wanawake, vijana, na makundi maalumu.

Ushiriki wa Tanzania unasisitiza nguvu yake inayokua na kujitolea kwake katika kushughulikia changamoto muhimu za kimataifa, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, umaskini, na usalama wa chakula.

Tanzania inatarajia kutumia jukwaa hili kuvutia ushirikiano na ufadhili kwa miradi mbalimbali kama vile matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati, usalama wa chakula, kilimo kilichozingatia mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Mkutano huu unatarajiwa kuimarisha hadhi ya kimataifa ya Tanzania na kuunga mkono malengo yake ya maendeleo kupitia ushirikiano wa kimataifa wa kimkakati.