January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azima jenereta Kigoma

Na Mwajabu Kigazi, TimesMajira Online, Kigoma

RAIS Samia Suluhu Hassani amezima umeme uliokuwa unatumia jenereta na kuwasha umeme wa gridi ya Taifa katika Wilaya ya Kasulu na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya umeme iliyowekwa katika maeneo yao.

Rais Samia alizima majenerata hayo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Kigoma.

Akizungumza akiwa wilayani Kasulu mkoani hapa, Rais Samia alisema wananchi wamepata umeme wa kutosha utakaowasaidia kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

Rais Samia aliwataka wakazi wa Kasulu

kulinda majenereta yaliyokuwa yakitumika awali, kwani yatatumika wakati wa dharura na kulinda miundombinu ya umeme iliyopo njiani inayofikisha umeme wilayani humo.

“Pamoja na kwamba tumezima jenereta zilizokuwa zinatumika, lakini tumeweka akiba na nawaomba jenereta hizi ni mali yenu watu wa Kasulu, pamoja na kwamba yanatunzwa na shirika la umeme (Tanesco), ni muhimu kuyatunza yasiharibiwe na kituo hiki kibaki kama kilivyo,” akusema Rais Samia.

Alisema maendeleo hayo ni kwa ajili yao na Serikali inafanya kwao na wanafanya kwa sababu wananchi waweze kufanya shughuli zao za kila siku za kimaendeleo katika wilaya yao hivyo waweze kulinda mali zilizopo kwa manufaa yao.

Alisema mkoa wa Kigoma upo pembezoni mwa nchi ya Tanzania wanaleta umeme wa uhakika ili wawekezaji waweze kwenda kwa wingi na kuwekeza katika mkoa huo, kama ni dhahabu ziweze kuchenjuliwa na wawekezaji kutoka nchi jirani.

Naye Waziri wa Nishati, January Makamba

alisema umeme huo utasaidia kuondoa gharama nyingi za uendeshaji, matengenezo na mafuta.

“Umeme wa gridi kufika kigoma kuna manufaa makubwa sana ya kiuchumi, Mkoa wa Kigoma kwa vituo vyetu hivi vya kuzalisha umeme kwa majenereta ni megawati 14, lakini umeme uliokuja kwa gridi sasa hivi ni wa megawati 20

Alisema kwa mwaka mafuta peke yake kwenye vituo vya kuzalisha umeme kwenye jenereta ni sh. bilioni 52 kwa mwaka, lakini mapato yanayopatikana ni sh. bilioni 14.

“Matumizi ya umeme wa jenereta yalikuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali. Mg 14 jenereta. Kwa mwaka gharama zilikuwa ni sh. bilioni 52. Mapato ni bilioni 14 kwa mwaka. Serikali ilitumia pesa nyingi kuliko mapato yake. Tulikuwa tunatumia mafuta lita 12,000 kwa siku,”alisema.

Katika hatua nyingine Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako ameiomba Serikali kutatua changamoto ya maji

barabara, umeme na upatikanaji wa mbolea jimboni kwake.

Akitoa salamu zake kwa Rais Samia jana wakati wa ufunguzi wa barabara ya Kidahwe- Kasulu na uwekaji jiwe la msingi barabara ya Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo, Profesa Ndalichako licha ya kuishukuru Serikali ameiomba itoe kipaumbele kwa barabara za Kasulu.

“Kwenye barabara niombe sana pamoja na shukrani ninazo zitoa lakini kwenye kazi ya barabara bado sana. Ukienda kwenye Kata ya Muhunga wakati wa mvua hakupitiki kabisa, tuombe suala la barabara katika mji wa Kasulu lipewe kipaumbele

“Barabara za kuunganisha Kata na Kata za Mitaani bado ni changamoto kubwa. Barabara nyingi hazina makalavati wakati wa mvua inakuwa ni adha kubwa, huwezi kuamini sehemu nyingine mitaani wananchi wanapanda mipunga kwenye barabara kwasababu hakuna njia ya maji kwenda,” alisema.

Kuhusu Maji, Ndalichako alisema licha ya kupatikana kwa wingi baada ya Makamu wa

Rais Dkt. Philip Mpango kumuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuchimba visima lakini usambazaji bado haujakamilia.

“Niombe sana usambazaji wa maji ukamilike ili wananchi waweze kunufaika, visima vimechimbwa tangu Septemba mwaka jana mpaka leo wananchi hawajasambaziwa maji,” alisema.

Alisema pamoja na nia ya Rais Samia ya kuona wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu, lakini upatikanaji wake ni changamoto kubwa akidai wananchi wanapanga foleni, mawakala wachache na kusababisha wananchi kukesha kutafuta mbolea.

“Lipo changamoto ya uandikishaji watu ili wapate mbolea. Ili mwananchi aweze kupata mbolea lazima awe na namba ya utambulisho.

“Wananchi ambao wamejiandikisha mpaka sasa ni zaidi ya 8,000 hawajapata namba za utambulisho maana yake hawa hawawezi kabisa kununua mbolea. Tunaomba namba za mbolea zipatokane na vituo viongezwe,” amesema.

Kuhusu umeme alisema “Mji wangu wa Kasulu una mitaa 108, mitaa 77 mpaka sasa mingi haijasambaziwa umeme wa Rea. Kwahiyo namuomba sana kaka yangu (Waziri wa Nishati, Januari Makamba) awaambie wananchi nini kinaendelea,” amesema.

Hata hivyo, Makamba alisema baada ya mkoa huo kuonganishwa kwenye gridi ya Taifa changamoto ya umeme mkoani humo inaenda kukoma.

Akijibu changamoto ya kuchelewa kutolewa namba za wanaojisajili kwa ajili ya kununua mbolea pamoja na uchache wa mawakala, Rais Samia alisema wataongeza mawakala baada ya wiki mbili, huku akitaja tatizo la kimtandao ndiyo chanzo cha kucheleweshewa namba zao.

Awali akitoa taarifa ya miradi ya barabara hizo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila alisema wakazi wa mkoa huo wataondokana na changamoto ya kukaa barabarani saa saba au siku nzima kipindi cha mvua badala ya saa nne kwa barabara ya lami.

Baada ya barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa Kilomita 260.6 kujengwa ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu hadi Manyovu inaunganisha Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza.

“Pia inaunganisha nchi jirani ya Burundi kupitia mpaka wa manyovu. Barabara hii imekuwa ikipitika kwa shida sana kipindi cha mvua,” amesema.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara kuu zinazounganisha mikoa na nchi jirani.

Alisema barabara hiyo itapunguza gharama za usafiri, usafirishaji, muda pamoja na kuimili mzigo wa kwenye magari.

“Kutokana na umbali mrefu wa barabara hii, usafiri kati ya Nyakanazi na Kigoma umekuwa ukichukua masaa karibia saba hadi zaidi ya siku moja kipindi cha mvua badala ya takribani masaa manne kwa barabara ya lami. Hali hii inasababisha adha kwa wasafiri na wasafirishaji wa mazao mbalimbali,” amesema