November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aweka jiwe la msingi ujenzi kituo cha Pamoja cha Forodha mpakani mwa Tanzania na Malawi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira onlin,Mbeya

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi kwenye mradi  wa ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha Kasumulu wilayani Kyela katika mpaka wa Tanzania na Malawi .

Jiwe hilo la msingi limewekwa Agosti 7, 2022 na Rais Samia katika mradi huo unaojengwa na Kampuni ya  China Geo-Engineering Corporation (CGC) na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Engineering Consultant Group      (ECG) kutoka Misri.

Akizungumza na wananchi wakati wa uwekaji wa jiwe hilo la msingi,Rais Samia amewaasa wananchi kuulinda na kuutunza mradi huo ili uwe endelevu kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ametoa pongezi kwa waliojenga mradi huo huku akisema ni matumaini yake kwamba atarudi kwa ajili ya kuuzindua ili uanze kuhudumia wananchi .

“Ombi langu ,naomba wananchi muulinde, mradi huu ni  wenu ,naomba mtoe  ushirikiano ,ulindeni pamoja na miundombinu yake ili ukae kwa kipindi kirefu na uweze kuchangia maendeleo ya Taifa letu.”amesisitiza Rais Samia

Aidha kabla ya kuweka jiwe la msingi katia kituo Kituo cha Pamoja cha Forodha,Rais Samia alitembelea kuona ujenzi wa jengo la abiria katika eneo hilo ambapo alipokea maelezo kuhusu jengo hilo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo wa Majengo Tanzania (TBA) Msanifu Majengo Daud Kandoro.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea maelezo juu ya jengo la abiria kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo wa Majengo Tanzania (TBA) Msanifu Majengo Daud Kandoro alipotembelea jengo hilo kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha pamoja cha Forodha Kasumulu wilayani Kyela mpakani mwa Tanzania na Malawi .