January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia awapongeza Kuwait

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online,Dar

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salaam za pongezi na kumtakia afya njema Amir wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Mishal Al Ahmad Al Jaber Al Sabah katika kuadhimisha miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo imeadhimishwa Februari 21, 2024.

Katika salaam zake za pongezi, Rais Samia amepongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa na nchi ya Kuwait katika maeneo mbalimbali ikijumuisha sayansi na teknolojia, huduma za afya na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla na kuiwezesha Kuwait kuwa moja wapo ya nchi zenye uchumi imara duniani na kituo maarufu cha kifedha, mitaji na uwekezaji.

Aidha Rais Samia ameeleza kuridhishwa na uhusiano imara uliopo baina ya Tanzania na Kuwait na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na Kuwait katika kuimarisha biashara, uwekezaji na maendeleo ya jamii kwa maslahi ya wananchi wa pande zote.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Kuwait kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya afya nchini ikiwemo msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali za Tanzania Bara na Zanzibar.

Ummy alitoa kauli hiyo aliposhiriki kama mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru na miaka 33 ya Siku ya ukombozi wa Kuwait yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 21 Februari 2024 na kuongozwa na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Kuwait imekuwa mshirika mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya hapa nchini ambapo tayari imetoa msaada wa mashine za ganzi kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Vifaa tiba katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Mashine za Watoto Wachanga zisizo na hewa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Handeni, Tanga unaofadhiliwa na Taasisi ya Abdullah Al Nouri ya Kuwait.

Balozi wa Kuwait nchini, Mubarak Mohammad Alsehaijan akizungumza wakati wa kuadhimisha miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo iliyoadhimishwa Februari 21, 2024 jijini Dar es Salaam.

Aidha aliongeza kusema mwaka 2023 Kuwait kupitia Kuwait Children Heart Association ilileta madaktari bingwa walioshirikiana na watalaam wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto 100 wa kipato cha chini.

“Tunaishukuru Kuwait kwa msaada wake katika Sekta ya Afya, pamoja na kutoa msaada wa mashine za ganzi, wameweza kusaidia vifaa vya upasuaji kwa watoto wanaosumbuliwa na vichwa vikubwa (Hydrocephalus) kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).” alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Mubarak Mohammad Alsehaijan alisema kuwa ushirikiano wa Kuwait na Tanzania umekuwa ukikuwa na kuimarika tangu mwaka 2015.

Kuwait itaeendelea kushirikiana na Tanzania kijamii, kisiasa na kiuchumi wakati wote.

“Tunapoadhimisha siku hii muhimu, mataifa yetu yanategemea kuanzia ushirikiano katika sekta ya michezo kati ya Mamlaka ya Michezo ya Kuwait na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ya Tanzania. Aidha, Balozi Alsehaijan aliongeza kuwa Kuwait itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Balozi Alsehaijan.

Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru na miaka 33 ya Siku ya ukombozi wa Kuwait yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa Shaib pamoja na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Tanzania na Kuwait zinashirikiana katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, maendeleo ya miundombinu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji ambapo kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.