February 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia awaonya Majaji na Mahakimu

*Awataka wasijigeuze Miungu Watu kwenye utoaji haki misingi waliyokubaliana katika sheria na kwenye Katiba, ataka wajikague nafsi zao, ahimiza wakae upande wa haki

Na Mwandishi WetuTimesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka majaji na mahakimu nchini wasiwe miungu watu, bali wahakikishe wanatoa haki kwa misingi waliyokubaliana katika sheria na kwenye Katiba ya nchi.

“Ni wasihi sana, niwaombe sana tusiwe Miungu Watu, mkatoe haki kwa misingi tuliyokubaliana kisheria na kikatiba. Ni wasihi tunapoanza Mwaka Mpya wa Mahakama zikagueni nafsi zenu na dhamira zenu.

Dhamirieni daima kukaa upande wa haki na kutenda haki.” Rais Samia alitoa angalizo hilo jijini Dodoma wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ikiwa ni kiashirio cha kuanza kwa Mwaka Mpya wa Mahakama.

Alisema kazi ya kutoa haki ni ya Mwenyezi Mungu ambaye ana jaala na kudra ambavyo pia uvitumia katika kumkadiria mwanadamu.

Alisema Mwenyezi Mungu mbali ya kutoa haki, lakini pia ana jaala anakujalia anachokipenda .

“Lakini pia ana kudra, unaweza ukawa unataka hiki, lakini akashusha kudra yake ukapata kikubwa au usipate kabisa kile ulichokita.

Nyie majaji na mahakami ni mawakala wa utoaji haki hapa duniani, lakini mmenyimwa jaala na kudra, sifa hizo hamna, kwa hiyo mnafanya kazi zenu kwa makubaliano yetu kisheria na katiba ya nchi,” alisema Rais Samia.

***Apongeza mafanikio ya mahakama

Katika hatua nyingine Rais Samia amepongeza mafanikio makubwa ambayo mahakama imeendelea kuyapata chini ya uongozi wa Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Alisema Mahakama ya Tanzania inaendelea kuwa kinara wa matumizi ya Tehama Afrika na vile vile imeendelea kuwa mfano mzuri kwa mfumo wa hakara kwa uchapaji wa hukumu.

Aidha, alipongeza watumishi wa mahakama kwa kufanyakazi kwa kuzingatia weledi, kuwasiliana kwa karibu na kushauriana na hatimaye kuleta matokeo yanayopimika.

Alisema wamefanya hivyo na kuwafanya wananchi kuridhishwa na huduma za mahakama kwa aislimia 88 kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya utafiti uliofanywa na REPOA mwaka 2023 na pengine ripoti ya mwaka 2024 asilimia hiyo inaweza kwenda juu zaidi.

Alimshukuru Jaji Mkuu kwa kutambua mchango wa Serikali kwenye maboresho yote inayoyafanya kwenye Muhimili wa Mahakama.

Kwa mujibu wa Rais Samia Serikali inafanya yote hayo kwa kuwa wanaaminika katika haki na wanapenda haki itamalaka.

Alisema akiangalia kauli mbiu ya mwaka huu Wiki ya Sheria inadhihirisha kuifanya Dira ijayo kuwa ya mipango ya kukuza haki nchini.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 hautakuwa rahisi kwa hiyo mahakama na wadau wake wajipange vema na wadau wengine kama ambavyo inafanya mahakamani.

Alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa inayomalizikia 2025 umekuwa na matokeo chanya katika maisha ya wananchi, kwani hali ilivyokuwa mwaka 2000 sivyo ilivyo leo.

“Mabadiliko hayo yapo dhahiri katika sekta za kiuchumi, maendeleo ya jamii na sekta ya kifedha hata kwenye sekta ya utoaji haki tumeshudia maendeleo makubwa,” alisema.

Alitoa mfano kuwa hakuna aliyekuwa akiwaza kuwa majengo ya mahakama yangeweza kuwa sehemu ya ya majengo mazuri sana yanayopendezesha miji.

Aidha, Rais Samia alisema sasa katika mahakama za Tanzania kusikiliza mashauri kwa njia ya mitandao ni jambo la kawaida, sio simulizi tena.

Alitoa mfano kuwa kwaa mwaka 2023 mashauri 172, 301 yalisajiliwa katika Mahakama za Mwanzo, aidha mashauri 70,714 yalisikilizwa na kumalizika kwa njia ya mtandao kuanzia Mahakama za Wilaya hadi Mahakama Kuu, ambapo baadhi ya mashahidi waliweza kutoa ushahidi wakiwa nchi mbalimbali duniani.

Alisema hatua hiyo imesaidia kuondoa usumbufu, usafiri na gharama. Aliongeza kwamba mageuzi na maboresho kwenye mahakama hayajatokea kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mipango madhubuti na hatua za makusudi.

Alisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya utekelezaji wa mipango iliyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25.

Alisema akiagalia sheria na dira mpya inayokuja ni jambo lililo dhahiri kuwa sauti za Watanzania kwa miaka 25 ijayo litakuwa ni Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

Alisema katika kufikia matamanio hayo Muhimili wa Mahakama utakuwa na mchango mkubwa na wanategemea utatimiza wajibu wake ipasavyo.

Alisema utekelezaji wa dira ijayo haitakuwa kazi nyepesi na hilo ni angalizo kwa Serikali, Bunge na Mahakama.

“Kwa mfano dira ijayo itaweka lengo la kuongeza pato la Taifa hadi kufikia dola bilioni 700 ifikapo 2050.

Ili kuweza kufikia hapo itatakiwa kuvutia sekta za kukuza uchumi ikiwemo kuvutia uwekezaji na biashara, kuvutia mitaji nchini na kukuza njia za ukusanyaji mapato nchi,” alisema.

“Tunakokwenda miaka 25 ijayo tunaenda kuwa taifa kama yalivyo mataifa mangine duniani litakalopungua matumizi ya fedha taslimu mkononi, lakini pia tunakwenda kupambana na mifumo ya fedha za mitandaoni,” alisema.

Alisema kutokana na hayo lazima wajipange na watu wetu wanaohusika na ya kisheria waangalie mambo haya. Alisema katika kuhakikisha maslahi ya nchi yetu yanazingatiwa kwenye mikataba itakayoingiwa ni lazima watumishi kwenye ofisi ya mwanasheria mkuu wawe na uwezo na ubobezi kwenye masharti ya kimkataba yanayogusa sekta za kiuchumi na uwezo wa kusimamia miakata hiyo.

Alisema ilani ya CCM 2025 iliahidi pia kuimarisha Tume ya Utumishi wa Mahakama ili iweze kusimamia maadili na nidhanu katika utumishi wa mahakama.

Alisema ni imani yake Serikali imejitadi kufanya vema katika kuwezesha Tume kufanya majukumu yake. Alisema Serikali inatambua katika kazi kuna haki na wajibu, kwa hiyo alisisitiza taasisi zinazoshughulika na haki jinai na haki madai kuleta ustawi na haki nchini.

Alisema kwa kuwa jaji mkuu ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amefanya wajibu wake kutetea haki ya majaji na mahakimu kwa kumkumbusha aangalie maslahi yao.

Alisema Serikali inatambua mazingira magumu ambayo watumishi wa mahakama wamekuwa wakiyafanyia kazi.

Aliongeza kuwa ili haki iweze kutamalaki na maslahi ya taifa letu yalindwe vema na wajibu wa Serikali kutengeneza mazingira mazuri na vivutio vya utendaji wa mahakama.

“Hivyo basi maombi yaliyowasilishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama yanaendelea kufanywa kazi hatua kwa hatua kwa kuzingatia hali ya uchumi na yatakapokamilika mtendaji mkuu wa mahakama atawajuza.

Ahadi yangu kwenu ni kuendelea kuangalia maslahi ya sekta hii muhimu,” alisema Rais Samia.