April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atoa msaada kwa  kituo kinachohifadhi wasichana waliokimbia ukatili

Fresha Kinasa TimesMajiraOnline,Mara.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa  msaada  wa vitu mbalimbali katika kituo cha’Hope Mugumu Nyumba salama kinachotoa hifadhi kwa Wasichana waliokimbia ukatili wa Kijinsia ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kilichopo Mugumu Wilayani Serengeti Mkoani Mara kwa  ajili ya kusherehekea sikukuu ya Eid El Fitri na mkono wa pasaka.

Msaada wa vitu hivyo ni pamoja na  mafuta ya kupikia, Vinywaji (soda), sukari, unga, kitowea, na mahitaji mbalimbali  ambavyo vyote vina thamani ya Shilingi Mil.4.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Kemirembe Lwota amekabidhi msaada huo katika kituo hicho ambacho kinamilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) Machi 31, 2025. Ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake wa dhati  kwa Watoto hao pamoja na Wilaya hiyo.
 
“Nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Wilaya ya Serengeti na Wananchi kwa ujumla, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kitendo hiki cha kiutu, kibinadamu na kidini kwa kutupa mkono huu wa Eid El Fitri na pasaka wana Serengeti pamoja na watoto hawa wanaolelewa katika kituo hiki cha Hope for Girls.”amesema na kuongeza kuwa.

“Tunamshukuru Sana kwa kutukumbuka, leo tumekuja kukabidhi vitu hivi katika kituo hiki ambacho kina Watoto wengine ni yatima wengine wamefanyiwa ukatili katika maeneo yao na wapo kwenye kituo hiki wakilelewa. Tumekabidhi, Mchele, mafuta soda, unga na vitu mbalimbali ambavyo Mheshimiwa Rais ametupa tukabidhi.”amesema.

“Vitu hivi  vinathamani ya Shilingi Mil. 4 ambayo Mheshimiwa Rais  ametupa serikali ya Wilaya ya Serengeti ili tuje kufanya kitendo hiki cha muhimu kabisa siku hii ya leo, lakini pia na mkono wa Pasaka kutoka kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa tunashukuru sana kwa upendo wake mkubwa na wakipekee kwetu sote.”amesema  DC Kemerembe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) Rhobi Samwelly amemshukuru Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake wa dhati wa kuwajali Watoto hao na kuwapa furaha ambayo haitafutika katika maisha yao.

“Tunao watoto wa kike 83 katika kituo cha Hope Mugumu Nyumba salama, na watoto wa kike 97 katika kituo cha Nyumba salama Kiabakari Butiama.Tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kuwajali Watoto hawa  kuleta vitu hivi katika vituo vyetu tunasema Rais wetu asante sana Mama kwa upendo wako kwetu.” amesema Rhobi na kuongeza kuwa.

“Hakika Watoto hawa  wamefurahi sana kwa upendo huu na   tutaendelea kumuombea kwa Mungu amjalie afya njema na baraka tele katika kutuongoza Watanzania. Tunashuhudia  Maendeleo makubwa na   mazuri sana ameendelea kutufanyia Watanzania tutaendelea kumpa ushirikiano wa dhati wetu wetu.”amesema Rhobi

Joyce Vicent akizungumza Kwa niaba ya Wasichana hao, amesema ni faraja na furaha  kwao  kuona wanakumbukwa na kuthaminiwa na kiongoizi Mkuu wa nchi. Ambapo wamemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo Kemirembe Lotwa kufikisha salaamu kwa Rais Dkt. Samia za shukrani na pia wanamuombea kwa Mungu  baraka, afya njema na heri katika utumishi wake wa kuliongoza Taifa.