Na Penina Malundo, Timesmajira
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Mashirika na Taasisi za Umma kuhakikisha yanawajibika ipasavyo katika kulinda na kuendeleza uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika hayo, na kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo ya kiuchumi.
Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa.
Amesema kuwa mageuzi makubwa yanayotekelezwa na Serikali kwenye usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya Umma yameanza kuonesha mafanikio, ikiwemo Mashirika 11 kati ya 13 yaliyokuwa na mtaji hasi kuhamia kwenye kundi lenye mtaji chanya, na Mashirika mengine nane katika hayo yaliyokuwa yanapata hasara sasa yameanza kupata faida.
Katika kuzidi kuongeza mchango wa Mashirika kwenye uchumi, Rais Dkt. Samia amemuagiza Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kuendelea kuwajengea uwezo watendaji na kuhakikisha mashirika yanaongeza ubunifu na kuimarisha matumizi ya TEHAMA.
Amemtaka Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya kuangalia namna ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika umiliki wa mashirika kupitia soko la hisa.

Rais Dkt. Samia pia amesisitiza umuhimu wa kutambua Mashirika na Taasisi ambazo hazitoi mchango wa fedha moja kwa moja kwa Serikali, bali huchangia kupitia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Aidha, idadi ya Mashirika na Taasisi zilizochangia imeongeza kufikia 213, huku kampuni zenye hisa chache za Serikali zikiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa, zikiwemo Twiga Minerals (Shilingi Bilioni 93.6), Airtel Tanzania (Shilingi Bilioni 73.9) na NMB Bank (Shilingi Bilioni 68.1). Akizungumza awali, Msajili wa Hazina Mchechu amesema kiasi cha Sh1.028 trilioni kimekusanywa kutoka katika jumla ya taasisi na Mashirika 213 (195 ya umma na 18 Kampuni zenye hisa chache).
“Hii inamaanisha kuwa Mashirika 57 hayajatoa gawio bado— ambayo ni asilimia 22 ya Mashirika yote.“Tutaendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Mchechu.

Kati ya Sh1.028 trilioni zilizokusanywa mwaka huu wa fedha, gawio kutoka Mashirika na Kampuni zinazofanya biashara ni asilimia 59 ya makusanyo yote.Aidha, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi imechangia asilimia 35, huku mapato mengineyo yanayojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yakichangia asilimia sita ya mapato yote.
“Takwimu hizi ni ushahidi wa mwelekeo chanya na matokeo ya juhudi za mageuzi ya kiuendeshaji tunayotekeleza kwa maelekezo yako, Mheshimiwa Rais,”amesema Mchechu.

Amesema pamoja na mafanikio yote bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya, linapokuja suala la maboresho ya kiutendaji na kiuendeshaji.
Mchechu amesema miongoni mwa kazi zilizopo mbele ni kuhakikisha idadi ya mashirika yanayochangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali inaongezeka.Pia, amesema inatakiwa kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali katika uendesha na Mashirika yanayojiendesha kwa hasara yanaondoka katika kundi hilo.

“ Mashirika yameendelea kutekeleza kwa kiu na msukumo mkubwa falsafa yako ya R4 ambapo ofisi yangu pamoja na Mashirika tumejikita katika R2 yaani Reforms and Rebuild,” amesema Mchechu.
Naye Waziri Prof. Kitila amehaidi kuendelea kuhakisha wizara yake inasimamia kikamilifu maono ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kutoa matokeo bora kwa maendeleo ya Taifa.

Katika mwaka ujao wa fedha 2025/26, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imejipanga kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha usimamizi na tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.
“Lengo letu ni kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi hizi zinaendelea kutoa matokeo bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” amesema Prof. Kitila.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge aifagilia RUWASA Tanga
Rais Samia kuanza ziara ya siku saba Simiyu na Mwanza
Msigwa awataka wazazi kuzungumza na watoto wao matumizi mabaya ya mtandao