November 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atekeleza miradi 9 barabara za lami Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

SERIKALI ya awamu ya sita kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetekeleza miradi 9 ya barabara za lami zenye urefu wa km 538.1 Mkoani Tabora katika kipindi cha miaka mitati ya Utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoani hapa Mhandisi Raphael Mlimaji alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana, ambapo ameeleza kuwa miradi hiyo ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alieleza kuwa miradi hiyo ya kimkakati inayogharimu zaidi ya sh bil 495 ni muhimu sana kwa uchumi wa wakazi wa Mkoa huo na Wilaya zake kwa kuwa inaunganisha Mkoa na Mikoa mingine ikiwemo nchi jirani.

Alifafanua kuwa kati ya miradi hiyo 9 miradi 4 imekamilika kwa asilimia 100 na mingine 6 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo iliyopo kwenye hatua za mwisho za manunuzi na upembuzi yakanifu.

Meneja alitaja miradi iliyokamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa km 85.4 iliyotekelezwa na Kampuni ya CHICO Engineering Co. Limited kwa gharama ya sh bil 117.94.

Miradi mingine ni barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa km 108 iliyotekelezwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) kwa kushirikiana na Kampuni ya LEA International na LEA Associates na AES Ltd ya Tanzania kwa gharama ya sh bil 158.8.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni wa Komanga-Kasinde wenye urefu wa km 108 uliotekelezwa na Kampuni ya China Wu Yi Company Ltd na Egis International kwa gharama ya sh bil 140.02.

Mradi wa nne ni ule wa Kazilambwa-Chagu wenye urefu wa km 36 uliotekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya STECOL na Mkandarasi Mshauri kampuni ya TECU kwa gharama ya zaidi ya sh bil 30 na kipande cha Ugansa-Usinge chenye urefu wa km 7.4 ambacho utekelezaji wake unaendelea kwa gharama ya sh bil 11.7.

Mhandisi Mlimaji alibainisha miradi mingine ya kimkakati kuwa ni pamoja na barabara ya Sikonge (Ipole)-Ruangwa ambapo kwa kuanzia watajenga km 10 za lami, kwa sasa wameanza na mita 600 kwa gharama ya sh bil 1.650.

Alitaja miradi iliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kuwa ni Mambali-Bukene-Itobo (km 1.1), Puge-Ziba-Choma ( km 109), Tabora-Ulyankulu (km 90.0) na Ujenzi wa Jengo la kupumzikia abiria (uwanja wa ndege Tabora) kwa gharama ya sh bil 24.6.

Alieleza mafanikio chanya ya miradi hiyo kuwa ni kukuza uchumi wa wananchi, Mkoa na nchi kwa ujumla, kupunguza gharama za uendeshaji magari kwa kuwa hayataharibika hovyo kama ilivyokuwa huko nyuma na kupunguza muda wa safari kwa wasafiri na usafirishaji bidhaa za wakulima na wafanyabiashara.

Kukamilika kwa miradi hiyo iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Mei 18 mwaka 2022 kumeanza kuleta neema kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Akieleza manufaa ya miradi hiyo Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema uzalishaji bidhaa za kilimo umeongezeka kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara kutoka mikoani na nchi jirani wameendelea kumiminika.  

Aliongeza kuwa mkoa huo umekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji na wageni wengi wameendelea kuanzisha biashara zao na kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo kujenga maduka makubwa, hoteli na nyumba za kulala wageni.