November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atatua adha ya watoto kutembea umbali mrefu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Siha

Mbunge wa Jimbo la Siha,Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel amesema kuwa Rais wa Samia Suluhu Hassan amewapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu wa kwenda shule watoto jimboni humo kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule kila kijiji.

Dkt. Mollel amebainisha hayo wakati akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni Siha ambapo amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili kupata elimu.

Amesema Rais Samia katika Jimbo la Siha ameupiga mwingi hususani kwenye kuboresha miundombinu ya elimu na madarasa mengi yamejengwa katika shule zilizokuwa zimechakaa na kuleta taswira mpya katika jimboni humo.

“Mpaka sasa tumebaki na vijiji vichache sana ambavyo havijapata shule ila naimani kubwa kwa dhamira ya kiongozi wetu kabla ya 2025 atakuwa ameweka mambo safi,”ameeleza Dkt. Mollel.

Aidha ameeleza kuwa serikali inaendelea kuhakikisha inaleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kuboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji pamoja na umeme ili kuwatia moyo wananchi.

Katika sekta ya afya amesema kuwa upatikanaji wa dawa umeongezeka ambapo kila watu 10 wanaopata dawa watatu ndio wanakosa dawa tofauti na ilivyo kuwa awali.

Dkt. Mollel amesema kuwa kabla ya kufanya mkutano wa Jimbo amechukua jukumu la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jimboni humo ili kuona imefikia wapi na kuhakikisha anatatua changamoto zote zilizopo katika kutekeleza miradi hiyo kukamilika.