December 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataka benki ziendelee kupunguza riba mikopo ya kilimo

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Mbeya

Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ameipongeza benki ya NMB kwa kuweza kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wakulima hadi asilimia tisa huku akisisitiza kuwa ikibidi riba hiyo ipunguzwe zaidi ili kulipa unafuu kundi hilo.

Rais Dkt. Samia amesema vijana wanaopewa mikopo hiyo bado wachanga kwenye shughuli za kilimo, hivyo kama watapewa mikopo yenye riba nafuu, itawapa muda ya kuweza kujipanga kabla ya kusimama kwa miguu miwili.

Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB Solo Mlozi (kushoto) akitoa maelezo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Ametoa pongezi hizo Agosti 8, 2023 wakati alipotembelea banda la NMB kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

“Nawashukuru NMB kwa kushusha riba kwa ajili ya kuwakopesha wakulima na kwa jitihada za kuiunga mkono Serikali kwa ajili ya kuongeza tija kwenye kilimo,endeleeni kupunguza riba ili wakulima na wananchi wetu waweze kufaidika zaidi,” amesema Dkt. Samia.

Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo na Biashara wa NMB Solo Mlozi alimueleza Rais Dkt. Samia kuwa kwa miaka miwili benki hiyo imetenga kiasi cha bilioni 40, kati ya fedha hizo bilioni 20 ni kwa ajili ya mikopo ya kuunga juhudi za Mpango wa Kuwaandaa Vijana na Wanawake kwa Kesho iliyo Bora (BBT).

Baadhi ya matrekta na power tiller zilizopo katika banda la NMB kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Huku kiasi cha bilioni 20 zingine ni kwa ajili ya mikopo ya ujenzi wa maghala ya kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno.

Mlozi amesema benki hiyo pia imepunguza riba kwa mikopo ya kilimo hadi kufikia asilimia tisa, nia ikiwa kumuwezesha mkulima kupata nafuu kwenye mikopo na tija kwenye kilimo.

Mlozi amesema wametoa mikopo ya zaidi ya bilioni 319 tangu walivyoanza kutoa mikopo ya riba ya asilimia tisa (single digit) Aprili 7, 2021. lakini wameweza kutoa mikopo ya kilimo trilioni 1.6 kwa miaka sita mfululizo.

“Kuthibitisha namna tulivyodhamiria kuwainua kiuchumi wadau wa kilimo, NMB ndiyo benki ya kwanza nchini sio tu kukopesha kiasi kikubwa, bali pia kushusha riba kwa mikopo ya kilimo, uvuvi na ufugaji hadi kufikia asilimia tisa, kwa mikopo hiyo inayoanzia 200,000 hadi bilioni moja kwa mtu mmoja mmoja, vikundi, taasisi, mashirika na Vyama vya Ushirika vya Wakulima (AMCOS),”ameeleza Mlozi na kuongeza kuwa

“Ndani ya miaka miwili hii, NMB tumetenga bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya mazao vijijini Ili kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao, ambako tayari zaidi ya bilioni saba kati ya hizo zimeshakopeshwa ndani ya mwaka huu pekee pia tumetenga bilioni 20 kuwezesha Program ya BBT, na mchakato wa kukamilisha hilo unaendelea baina yetu na Wizara ya Kilimo,” amesema Mlozi.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika banda la NMB kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.