April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia asisitiza amani nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuendeleza juhudi za kudumisha amani na kuzingatia jukumu lao la kiroho katika jamii.

Rais Dkt. Samia alitoa kauli hiyo leo wakati wa Baraza la Eid El-Fitr lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) mjini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kusambazwa kwa vyombo vya habari, iliyonukuhu hotuba ya Rais Dkt. Samia akiwasihi viongozi wa dini kutotumia majukwaa ya ibada kuhubiri siasa au kueneza ajenda za kisiasa zinazoweza kuathiri amani ya nchi.

“Muwadhibiti wachache walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki dhidi ya Serikali yao,” alisema Rais, akiongeza kwamba migogoro na mifarakano haitakayeza kumalizika kwa mshindi.

Aidha, Rais alisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia yeyote anayejitahidi kuchochea chuki au kuvunja amani, na kwamba ni jukumu la kila mtanzania kulinda amani nchini. “Jukumu la kusimamia amani ni la Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama lakini pia ni jukumu la wananchi wote,” alibainisha.

Rais Dkt. Samia alikumbusha Waislamu kuendeleza heshima na umoja waliokuwa nao katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakati wanaposherehekea Eid El-Fitr, na ilikuwa muhimu kuhifadhi ibada zao.

Katika muktadha wa Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa wadau wa kisiasa kutimiza wajibu wao na kutopuuza amani kwa sababu ya itikadi za kisiasa.

“Milango ya Serikali iko wazi kusikiliza madai ya wadau wa kisiasa kupitia majukwaa mbalimbali,” alisema, akitaja hatua za mageuzi katika mfumo wa uchaguzi kama vile kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Rais Dkt. Samia alihitimisha kwa kuwaasa viongozi wa dini na wananchi wote kuendelea kufanya kazi pamoja ili kudumisha amani na umoja katika nchi.