April 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ashiriki mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi kwa njia ya mtandao

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na hatua za Mpito za Haki katika kukabiliana na athari za tabianchi, uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil, Luiz Inacio Lula Da Silva, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na umehusisha viongozi kutoka mataifa 17 pamoja na wenyeviti wa mikutano ya awali ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) kwa miaka ya 2023 (Umoja wa Falme za Kiarabu), 2024 (Azerbaijan), na 2025 utakaofanyika Belem, Brazil.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuweka msukumo mpya katika kufanikisha ajenda ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia barani Afrika, hasa kwa watu zaidi ya milioni 950 ambao bado hawana huduma hiyo. Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), utakaofanyika mwezi Novemba 2025 jijini Belem, nchini Brazil.