*Asema katika kipindi cha miaka minne halmashauri 122 zimepata majengo, huduma maji, umeme, elimu, barabara zafikia wengi nchini
Yusuph Mussa na Hadija Bagasha, Timesmajira, Lushoto, Bumbuly
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwa ya mafanikio mkoani Tanga, huku akiendelea kufungua miradi iliyotekelezwa na fedha ambazo Serikali ilipeleka mkoani humo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuly, mkoani Tanga.
Akizungumza mara baada ya kuzindua jengo hilo, wilayani Bumbuly jana, Rais Samia, alisema safari ya ziara yake wilayani humo, ni kwenda kuangalia matumizi ya fedha walizozipeleka kwa ajili ya ujenzi w ajengo hilo.
Alishukuru halmashauri, wafanyakazi, wakandarasi, washauri kwa ujenzi mzuri wa jengo hilo. “Lakini shukrani kubwa sana kwa TAMISEMI kwa kusimamia mpaka jengo limetimia.”
Alisema na jambo zuri ni kwamba watumishi wote watakuwa humo ndani. Alitoa shukrani kwa wana Bumbuly wakiongozwa na Mbunge wao, January Makamba.
Rais Samia alisema katika kipindi cha miaka minne halmashauri 122 zimepata majengo mapya na mazuri, na kuongeza kuwa kama wabunge watatu wa wilaya ya Lushoto walivyosema, huduma za jamii ikiwemo maji, umeme, elimu, barabara vimewafikia wananchi.
Wakati huo huo, Rais Samia, amesema anamrudisha kwa Mama Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba, kwani kilichotokea ni sawa na Mama kumuonya mwanawe.
Alisema hayo hayo jana wakati anahutubia wananchi wa Wilaya ya Lushoto kwenye Uwanja wa CCM wa Sabasaba mjini Lushoto.
Alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge huyo kutoa neno la shukrani kwa Rais Samia, namna alivyomtendea akiwa Waziri wa Nishati, na baadae Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, lakini pia huduma za jamii na maendeleo kwenye jimbo lake.
“Sisi wamama mnatujua, mtoto akikukera unampiga kikofi na kumfichia chakula, si ndiyo. Sasa mwanangu (January) nilimpiga kikofi nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa Mama” alisema Rais Dkt. Samia na kumwita January na kumkumbatia.
Naye Mbunge wa Bumbuly, Makamba alisema alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuweza kuwaondolea kilio cha zaidi ya miaka 20 cha barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi- Old Korogwe, ambapo tayari mipango ya kuweka lami inafanyika.
“Sisi watu wa Bumbuli kwa muda mrefu sana tumekuwa tunazungumzia barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi na Korogwe, kwa miaka 20 sasa imekuwa ndiyo kilio chetu Juzi karibu wiki tatu zilizopita tumepata taarifa ya Waziri wa Ujenzi kuwa wewe Waziri kuwa umetoa kibali sasa kwamba barabara hiyo itangazwe na kujengwa ujenzi kwa kiwango la lami.
“Mheshimiwa Rais utakuwa umeacha historia kubwa sana katika Milima hii ya Usambara. Kama unavyofahamu, barabara ya Lushoto ni moja, na sasa tutakuwa na barabara mbili, kwani huko nyuma mvua zilinyesha kukatokea maporomoko ya mawe (Soni- Mombo), na kufanya barabara ishindwe kupitika kwa wiki mbili, na kufanya vitu vipande bei, hivyo barabara hii itatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi na wakulima wetu” alisema Makamba.
Makamba alisema anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kumteua kuwa Waziri. Kwanza Waziri wa Nishati na baadae Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, hiyo kwake ni historia na haitafutika kwenye maisha yake hadi atakapoingia kaburini
” Naomba nishukuru sana kutoka sakafu ya moyo wangu kwa kuniamini mimi, kwanza kwa kuniteua kuwa Waziri wa Nishati, na baadae Waziri wa Mambo ya Nje. Ni heshima kubwa ambayo haitafutika katika uhai wa maisha yangu. Katika kipindi nimefanya kazi na wewe nimejifunza sana, na nimeerevuka sana kutokana na uongozi wako.
“Lakini kabla ya hapo nilikuwa Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira) katika ofisi yako, na wewe ndiyo umenifundisha kazi, sababu tulifanya kazi wote miaka minne, na hiyo ilikuwa nafasi yangu ya kwanza ya uwaziri. Kama nina uerevu nilionao kwenye utumishi wa uwaziri, basi umetokana na mkono wako Mheshimiwa Rais naomba nikushukuru, na hii nitaenda nayo kaburini kwangu” alisema Makamba.
More Stories
Ziara ya Rais Samia yaanza kwa kishindo mkoani Tanga
Gambo: Rais Samia amefanya makubwa Jimbo Arusha Mjini
Samia ajitosa madai yawalimu wasio na ajira