Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Kaliua
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka zaidi ya sh bil 6 Wilayani Kaliua Mkoani Tabora ili kuboresha sekta ya elimu kupitia program za SEQUIP, EP4R na BOOST.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Japhael Lufungija ameeleza hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.
Amesema kuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri ilipokea jumla ya sh bil 6.63 kupitia program za SEQUIP, EP4R na BOOST ili kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ya awali , msingi na sekondari .
‘Tunamshukuru sana Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika halmashauri yetu, tumejenga shule mpya za msingi na sekondari na mabweni ya wanafunzi ya kutosha’, ameeleza.
Lufungija ametaja kazi zilizofanyika kuwa ni ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika shule ya sekondari Usimba (sh mil 110), ujenzi shule ya sekondari Mnange (sh mil 603.8) na ujenzi shule ya sekondari Mwaharaja kwa gharama kama hiyo hiyo.
Miradi mingine ni ujenzi wa shule ya sekondari Isanjandugu (sh mil 603), ujenzi shule ya sekondari Makingi (sh mil 603.8) na ujenzi shule ya sekondari Makubi (sh mil 603) na ujenzi wa shule ya sekondari Dkt Batilda Burian (sh bil 1,100).
Lufungija amebainisha miradi mingine ya elimu iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa nyumba ya mtumishi sekondari ya Sasu ( sh mil 110), ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika sekondari ya Sasu (sh mil 398) na Usimba (sh mil 398).
Mabweni mengine 2 yamejengwa katika shule ya sekondari Mkindo kwa gharama kama hiyo hiyo na nyumba ya walimu ya familia 2 shule ya sekondari Nhwande kwa gharama ya sh mil 110 na sekondari ya Mkindo sh mil 294.
Aidha sh mil 10 zimetumika kumalizia ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Mwongozo, na kubainisha kuwa miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha.
Mwenyekiti ameongeza kuwa kwa fedha za EP4R wameweza kukamilisha ujenzi wa bweni la shule ya sekondari Usimba ambalo limegharimu sh mil 25.1 ikiwemo ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Kashishi na kukamilisha madarasa yote.
Kupitia mradi wa BOOST amesema kuwa wamejenga shule mpya ya msingi katika Kijiji cha Maboha (sh mil 361.5), Kijiji cha Ibambo (sh mil 361.5), madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo shule ya msingi Malanga (sh mil 91) na vyumba 3 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo shule ya msingi Ilugu (sh mil 91.2).
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba