Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza ajira mpya 300 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kufanya jumla ya ajira zote kufikia 1,896 kutoka 1,596 zilizotangazwa awali.
Nyongeza hiyo imetokana na ombi la TRA la kuongeza nafasi za ajira 300 ambazo zilikasimiwa kwenye Bajeti ya Mwaka wa Fedha ujao wa 2025/2026 kujazwa kwenye mchakato wa ajira uliohitimishwa hivi karibuni ambapo ombi hilo limeridhiwa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kusainia na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Moshi Jonathan Kabengwe kwa niaba ya Kamishna Mkuu imeeleza kuwa waajiriwa wapya wa TRA 1,896 watapatiwa barua za za ajira hii leo tarehe 28.05.2025 kupitia barua pepe zao.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TRA Wasailiwa 1,896 ambao wamefaulu na wameitwa kazini wanatakiwa kufika katika kumbi walizopangiwa tarehe 02 Juni, 2025 saa 1:00 asubuhi bila kukosa wakiwa na nyaraka muhimu kama zilivyoainishwa kwenye barua pepe zao.

Mamlaka inawashukuru waombaji wote walioonesha nia ya kufanya kazi na Mamlaka ya Mapato Tanzania, na inawatakia kila la kheri katika ujenzi wa Taifa aidha, waombaji 4,429 ambao walishiriki usaili wa mahojiano na hawakufanikiwa kuitwa kazini, taarifa zao zitahifadhiwa kwenye kanzidata ya Mamlaka kwa matumizi ya baadaye.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza nafasi za kazi zipatazo 1,596 mwanzoni mwa mwezi wa Februari 2025, ambapo ilipokea jumla ya maombi ya kazi 135,027 kati yao 113,023 waliitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika baada ya kukidhi vigezo na usaili huo uliofanyika tarehe 29 na 30 Machi, 2025. Wasailiwa waliofanikiwa kwenye usaili wa kuandika waliitwa kwenye usaili wa mahojiano uliofanyika tarehe 12 hadi 14 Mei, 2025, ambapo wasailiwa 6,325 walifanya usaili huo.
More Stories
Prof.Mbede:Nishati ya umeme wa Sola imepunguza vifo vya wajawazito
Rais Samia apongezwa kuanzisha bima ya afya kwa wote
Serikali yajipanga kudhibiti matumizi yasiyo sahihi kuelekea uchaguzi mkuu