Amtaja kama Kiongozi wa Amani na Maendeleo
Na Mwandisihi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na duniani kote kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Papa Francisko, kilichotokea leo Jumatatu ya Pasaka huko Vatican.
Katika ujumbe wake wa maombolezo, Rais Samia amesema amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa kiroho, akimtaja kama “mwalimu na kiongozi aliyefundisha na kuhimiza ustawi na maendeleo ya watu pamoja na kudumisha amani” katika kipindi chake cha miaka 12 ya kuliongoza Kanisa Katoliki duniani.
“Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisko. Katika kipindi chote cha miaka 12 akiwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisko ameishi maisha yake kama mwalimu na kiongozi aliyefundisha na kuhimiza ustawi na maendeleo ya watu pamoja na kudumisha amani,” alisema Rais Samia katika taarifa yake rasmi.
Rais Samia aliongeza kuwa kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatuma salamu za rambirambi kwa waumini wote wa Kanisa Katoliki na kwa familia ya Vatican.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema Peponi. Amina,” alihitimisha.
Papa Francisko, ambaye alizaliwa Jorge Mario Bergoglio nchini Argentina, alikuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, na alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini. Uongozi wake ulitambulika kwa msisitizo wa upendo, unyenyekevu, na kujali masikini.
Kifo chake kimetikisa jamii ya kimataifa, huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakiungana na Wakristo kote duniani kumwombea apumzike kwa amani na kuenzi urithi wake wa kiroho.
More Stories
Papa Francis afariki Jumatatu ya Pasaka akiwa na miaka 88
Kanisa la Shincheonji la Yesu nchini Ufaransa lakanusha ripoti ya Le Parisie
Vyombo vya ulinzi na usalama Mbeya,Benki kuu kushirikiana kutatua changamoto za utapeli mtandaoni