December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MAPAMBANO dhidi ya rushwa nchini hapa yana historia ndefu. Tangu tulipopata uhuru mwaka 1961, rushwa ilibainishwa kama mojawapo ya vikwazo vikuu vya maendeleo na ustawi wa Taifa na wananchi wake.

Hivyo, Serikali kwa nyakati na awamu tofauti tofauti, imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na vitendo vya rushwa.

Mathalan, chama cha TANU kilipinga rushwa, na katika ahadi za
wananchama, kilimtaka kila mmoja kuapa kuwa “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”.

Ahadi hii imeendelea kuwepo katika ahadi za mwanachama wa
CCM.

Aidha, mwaka 1996 Tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba iliundwa ili kuchunguza vitendo vya rushwa vilivyoonekana kushamiri kwa wakati huo, licha ya hatua mbalimbali zilizokuwa zikichukuliwa na Serikali. Taarifa ya Tume hiyo ilibaini kuwa, rushwa ilikuwa imeenea katika sekta zote kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo:

Urasimu katika upatikanaji wa huduma muhimu za jamii;
kutokuwepo kwa usimamizi na uwajibikaji wa viongozi katika maeneo yao ya kazi; uhaba wa bidhaa na huduma muhimu za jamii; kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika kupambana na rushwa; na vyombo vya kupambana na rushwa kutowajibika ipasavyo.

Tume hiyo pia ilibaini kuwa rushwa ilikuwa imeshamiri sana nchini
kutokana na baadhi ya viongozi kujihusisha na vitendo vya rushwa. Hivyo, Tume ilipendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, kujenga uadilifu na kuwataka viongozi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kutokomeza rushwa nchini.

Licha ya hatua hizo, vitendo vya rushwa bado vinaonekana katika sekta mbalimbali hadi hivi sasa. Wananchi bado wana malalamiko mengi juu ya rushwa na kunyimwa haki.

Akizungumza juzi kwa niaba ya kt. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024 wa Viongozi wa TAKUKURU, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, anasema taarifa za kila mwaka za TAKUKURU na PPRA zinathibitisha haya.

“Mathalan, taarifa ya ukaguzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa taasisi 44 za umma zilizokaguliwa mwaka 2022/23, inaonesha zabuni 15 zenye thamani ya shs 67.27 bilioni zilitolewa kwa kutumia maelezo ya zabuni (tender
specifications) yenye kubagua baadhi ya wazabuni.

Wzabuni walichaguliwa (shortlisted) na kupewa mikataba 25 yenye thamani ya billioni 56.70 pasipo kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni, majadiliano ya mikataba 23 ya taasisi 7 yenye thamani ya billioni 64.51 yalifanyika bila kuwepo kwa mpango wa majadiliano (negotiation plan).

Mikataba 60 yenye thamani ya billioni 54.07 ilisainiwa pasipo kuidhinishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mikataba 10 ya manunuzi kwenye taasisi 5 yenye thamani ya billioni 7.48 iliongezwa muda bila kufuata utaratibu.Ni wazi kuwa dosari hizi katika taratibu za manunuzi zinaashiria uwepo wa rushwa.

Hivyo, ni vema TAKUKURU ifanyie kazi taarifa hizi na kuchukua hatua stahiki,pia ni muhimu viongozi kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kweli dhidi ya rushwa.

‘Viongozi tunaposhindwa kutimiza wajibu wetu,rushwa inashamiri na kuwafanya wananchi kukosa imani na Serikali yao, husababisha upotevu wa rasilimali za umma na kurudisha nyuma jitihada za maendeleo,” anasema Dkt. Mpango na kuongeza;

“Kutokana na hayo, ninaunga mkono kauli mbiu ya mkutano huu inayosema “Kuzuia rushwa ni kujumu lako na langu: tutimize wajibu wetu” ,kwa kuwa inatukumbusha wajibu na dhamira yetu katika kuzuia na kupambana na rushwa kwa nguvu zote katika maeneo yetu ya uwajibikaji,” .

Katika hili, napenda kurejea maneno ya Rais Dkt. Samia
alipohutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika, Julai 11, 2023 hapa jijini Arusha, aliposema,”Tunataka Dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika sio salama kwa wala rushwa, na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya wala rushwa na sio mikutano, makongamano na maneno peke yake”.

Anaipongeza TAKUKURU kwa hatua inazochukua mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini,na kwa mafanikio ambayo yamepatikana katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa Taarifa ya TAKUKURU ya Mwaka 2022/2023, pamoja na
mambo mengine,imefanikiwa kuokoa kiasi cha takribani bilioni 172.3, kukamilisha uchunguzi wa majalada 900, ikiwemo uchunguzi wa majalada 21 ya rushwa kubwa yenye thamani ya zaidi ya billioni 92,na Dola za Marekani 439,030.60.

Pia kufungua kesi mpya 600 ambapo Jamhuri ilifanikiwa kushinda kesi 336 kati ya kesi 496 zilizoamuriwa mahakamani, ikiwa ni sawa na asilimia 67.7 ya kiwango cha kushinda kesi.

Anasema licha ya mafanikio hayo, bado rushwa ipo na ameitaka TAKUKURU na wote kuongeza bidii katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

Anasema uadilifu wa viongozi na watumishi wa umma ni sharti muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Aidha anasema kiongozi anapaswa kuwa ni mtu asiyetiliwa mashaka kuhusu uadilifu na uwezo wake wa kiuongozi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa umma.

Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma ya Mwaka 1995 Toleo la Mwaka 2020 (The Public Leadership Code of Ethics Act, 1995, R.E 2020) katika Kifungu cha 6 (1) (a) inaeleza Kanuni muhimu za kuzingatiwa na viongozi wa umma kuwa ni pamoja na uaminifu,huruma, utimamu wa akili,kiasi na kujiepusha na ulevi
(temperance).

Pia uadilifu wa kiwango cha juu kabisa katika jamii ili kujenga imani ya wananchi na hivyo kuifanya Serikali itekeleza wajibu wake kwa malengo, uadilifu na bila upendeleo.

“Kwa ajili hiyo ninawataka viongozi wa TAKUKURU mliopo hapa na viongozi wote wa umma, kuonesha mfano bora katika mapambano dhidi ya rushwa, kwa kuboresha utoaji wa huduma, kuondoa mazingira na vishawishi vya rushwa katika maeneo ya kazi, na kuzingatia masharti ya Sheria na Kanuni za Maadili katika utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku ikiwa pamoja na kutoa taarifa za kweli za mali tunazomiliki na jinsi zilivyopatikana,”anasisitiza Dkt.Mpango.

Anasema Serikali inaendeleza pia mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwekeza katika ujenzi wa taasisi imara za haki jinai ili kupambana na makosa ya jinai ikiwemo rushwa.

Anasema katika hili, Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa upande wa rasilimali fedha na rasilimaliwatu ili kutekeleza wajibu wake wa kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Pamoja na ajenda zitakazojadiliwa katika Mkutano huu, itafaa pia mkutano huu uangazie na kuzingatia mambo muhimu yafuatayo;

“Jambo la kwanza, ni lazima viongozi na watumishi wa TAKUKURU ninyi wenyewe kuwa mfano wa kuigwa kwa mienendo mizuri, kufuatilia tuhuma mbalimbali kwa umakini na bila upendeleo kama inavyostahili heshima ya kiongozi na afisa anayepamabana na rushwa.

Ni lazima muonekane kufanya maamuzi kwa haki na na
kutumia madaraka yenu kutatua kero za wananchi kwa manufaa ya umma na siyo binafsi.

Aidha, jukumu la kupambana na vitendo vya rushwa ni zito na linalohitaji kutekelezwa kwa ujasiri, uaminifu na uzalendo wa hali ya juu. Kwa kupitia mkutano huu muhimu, ninatoa wito kwenu kuzingatia kuwa ufanisi wenu utatokana na namna mnavyojituma kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kufanya kazi kwa misingi
ya sheria, kanuni na taratibu,” anasema Dkt. Mpango na kuongeza;

“Jambo la Pili; ni umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kuchunguza, kuzuia na kuadhibu wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa mujibu wa sheria.

“Ningependa kuona mnatumia mkutano huu kubainisha udhaifu katika sheria na kanuni za kupambana na rushwa, na kupendekeza marekebisho kwa lengo la kuimarisha uchunguzi, usimamizi wa kesi, na viwango vya adhabu,ili kuhakikisha adhabu kali zinatolewa kwa kila atakayepatikana na hatia bila kujali hadhi au wadhifa wake. Vilevile, hakikisheni Ofisi zote za TAKUKURU nchini zinaunganishwa na mifumo ya TEHAMA,”.

Taarifa ya TAKUKURU ya mwaka 2022/2023 inaonesha
kuwa bado zipo Ofisi 50 ambazo pamoja na kuwa katika majengo ya TAKUKURU hazijaunganishwa na mfumo wa ndani wa TEHAMA. Pamoja na uhaba wa rasilimali fedha, uwekezaji katika mifumo hiyo imara ya ni muhimu katika utendaj kazi.

Hivyo, ni muhimu Mkutano huu ukaangazia suala hili na kuhakikisha
mifumo ya TEHAMA inasomana na ile ya taasisi nyingine hususani zile za haki jinai.

Jambo la tatu,watumishi wa TAKUKURU wanaotekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa, ni muhimu kuhakikisha wanajengewa uwezo na mbinu za kisasa za uchunguzi na uendeleshaji wa kesi za rushwa.

Aidha, ni muhimu kuhakikisha watumishi wa TAKUKURU wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni, pamoja na watoa taarifa kutambuliwa na kulindwa wawapo kazini au nje ya kazi, ili kuepuka kuhatarisha maisha yao.

Jambo la nne,ni kuhusu vitendo vya rushwa katika mchakato wa uchaguzi,” Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, nawakumbusha viongozi na watumishi wa TAKUKURU tujidhatiti kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vina madhara kwa maendeleo ya Taifa. Viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa, si tu kwamba hawawezi kukemea vitendo vya rushwa bali pia hawawezi kutatua kero za wananchi na kusimamia vema miradi ya maendeleo,”.

Katika msingi huo,amewataka wajiandae kikamilifu kukabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,”Mpige darubini zaidi kwenye matumizi ya mitandao na simu katika kuhamisha pesa za rushwa,”.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya taasisi za umma zinazopata hati inayoridhisha imeongezeka, hali ambayo inayoashiria uzingatiaji wa Sera, Sheria na Kanuni zilizowekwa kuhusu usimamizi wa rasilimali za umma. “

Hata hivyo, anasema taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinaonesha kujirudia kwa maeneo ambayo yanahitaji juhudi za makusudi, ikiwemo kuzingatiwa kwa taratibu za
ununuzi, na uwajibikaji kwa fedha zilizotolewa kwa matumizi ya maendeleo na ya kawaida.

Vilevile, utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayogharimu fedha nyingi za walipa kodi imeonekana kugubikwa na viashiria vya rushwa. Kutokana na vitendo hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo umekosa ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha. Kutokana na hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2024 katika
taarifa yake, alieleza kuhusu miradi iliyokaguliwa na ambayo ilibainika kukosa ubora na kuomba TAKUKURU kufanya uchunguzi wa miradi hiyo na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

“Nami kupitia jukwaa hili, nawakumbusha TAKUKURU kutekeleza agizo la Rais la kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wasimamizi wa miradi hiyo watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au ubadhirifu katika miradi hiyo iliyobainishwa.

Jambo la sita; ni kuhusu rushwa katika utoaji haki. Mwaka 2023, REPOA ilitoa taarifa inayoonesha kuanza kupungua kwa vitendo vya rushwa katika mahakama za juu.

Hata hivyo, Taarifa ilionesha kuwa bado kuna vitendo vya rushwa katika Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo ambako ndiko wananchi wengi wanakotafuta haki zao. Nashauri Mkutano huu usaidie kubuni mbinu na mikakati ya kukabiliana na rushwa katika mahakama za chini, mabaraza ya ardhi, na vyombo vingine vya haki jinai ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao.

TAKUKURU pia, ifanyie kazi mapendekezo ya taarifa ya haki jinai yanayohusu rushwa. Hivyo, mikakati mtakayoweka izingatie pia umuhimu wa elimu kwa jamii ili kuleta mwamko miongoni mwa wananchi, ili wao pia waweze kushiriki kikamilifu katika mapambano
dhidi ya rushwa.

Jambo la saba,anasema ni kuhusu ushiriki wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Vyombo vya habari vina na mchango mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuibua taarifa kuhusu maovu mbalimbali ikiwemo rushwa. Hata hivyo, zipo tuhuma kwad baadhi ya vyombo vya habari vikidaiwa kutumika kupotosha habari au kutoa habari zenye mrengo
fulani.

Kitendo hiki licha ya kuwa kina harufu ya rushwa, kinaweza kuwa na madhara makubwa katika jamii kwa kuikosesha jamii haki ya kupata habari ambazo zinaweza kuwa na manufaa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Napenda kutoa wito kwa vyombo vya habari kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa kwa kuandika taarifa za kiuchunguzi ili kufichua vitendo vya rushwa na kusaidia vyombo vya dola kufanya kazi yake, pamoja na kuelimisha jamii.