May 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia amteua Mkurugenzi Mtendaji TANESCO

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko katika safu ya uongozi kwa kuwateua na kuwahamisha viongozi mbalimbali wa serikali, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi katika maeneo husika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uteuzi na uhamisho huo unahusisha wakuu wa wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi wa mashirika ya umma.

Katika mabadiliko hayo:

  • Albert Gasper Msando amehamishwa kutoka Wilaya ya Handeni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
  • Japhari Mghamba Kubecha amehamishwa kutoka Wilaya ya Tanga kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni.
  • Dadi Horace Kolimba amehamishwa kutoka Wilaya ya Karatu kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga.
  • Lameck Karanga Nganga ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, akitokea nafasi ya Katibu Tawala wa wilaya hiyo hiyo.
  • Bahati Migiri Mfungo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu, ambapo awali alikuwa Afisa Tarafa ya Mbuguni, Wilayani Arumeru.
  • Lazaro Jacob Twange ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), nafasi aliyopata baada ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
  • Andrew William Massawe ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ambaye amemaliza muda wake.

Uteuzi huu unaonyesha dhamira ya Rais Samia kuendeleza mabadiliko ya kiutendaji yanayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na kuimarisha taasisi za umma kwa kuzingatia sifa na uzoefu wa watumishi husika.