Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani mwalimu Fakii Raphael Lulandala amesema kwa muda wa miaka mitatu na nusu aliyokaa madarakani Rais Samia Suluhu Hassan amefanikisha maendeleo makubwa kwenye wilaya hiyo.
DC Lulandala ameyasema hayo Septemba 8 mwaka 2024 kwenye ziara ya Katibu wa NEC – Itikadi Uenezi na Mafunzo CPA, Amosi Makala alipofanya ziara mji mdogo wa Mirerani.
Lulandala alisema kabla ya Rais Samia hajaanza kuongoza Tanzania, kwenye wilaya ya Simanjiro kulikuwa na vijiji 21 vyenye nishati ya umeme na sasa vijiji vyote 56 vina umeme.
“Kwenye miaka 60 ya uhuru wa nchi yetu kulikuwa na vijiji 21 vyenye umeme ila kwa miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Rais Samia vijiji 35 vikapatiwa umeme,” alisema Lulandala.
Alisema kwenye huduma za afya wananchi wa Simanjiro wamenufaika na uongozi wa Rais Samia kwani vituo vya afya vilikuwa vitatu pekee vya Orkesumet, Mirerani na Naberera.
“Ndani ya miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Rais Samia hivi sasa kuna vituo nane baada ya vitano kujengwa na vingine viwili vitakamilika kabla ya kufika kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema wachimbaji wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa maji, zahanati na barabara.
Ole Sendeka alisema wachimbaji wa madini ya Tanzanite wanakabiliwa na changamoto hizo hivyo kupitia CCM ambacho ni chama kinachotawala kwenye serikali ya awamu ya sita kisimamie changamoto hizo.
Alisema wachimbaji hao hawana mahali pakupata matibabu, kuna changamoto ya maji na pia miundombinu ya barabara ni mibovu.
“Hata hivyo, tunaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya ya Simanjiro,” alisema Ole Sendeka.
Mbunge wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amesema wafugaji wa wilaya ya Ngorongoro wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuruhusu wafugaji waendelee na shughuli zao za ujenzi wa Taifa.
Ole Millya alisema anamshukuru Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia jina lake kupitishwa kugombea ubunge wa Afrika Mashariki kupitia chama hicho.
Makala akizungumza baada ya kusikiliza kero na changamoto hizo ndani ya migodi ya madini ya Tanzanite amesema zitatatuliwa.
Makala akampigia simu Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa ambaye ameahidi kujengwa kwa zahanati yenye hadhi ya kituo cha afya.
“Tutatenga fedha Sh200 milioni kwenye mwaka huu wa fedha ili kuanza ujenzi wa majengo na kufikisha karibu huduma za afya kwenye makazi au kazini kwa jamii,” alisema Mchengerwa.
Kwenye sekta ya madini Makala akamtaka Naibu Waziri wa Madini Dk Kiruswa amesema biashara, kusanifu na kuongeza thamani madini ya Tanzanite itaendelea kuwa Mirerani.
Dkt. Kiruswa alisema kuhusu suala la soko na mnada wanatarajia kufanya mji mdogo wa Mirerani mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wa maji kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Arusha (AUWSA) CPA John Ndetiko amesema wameweka utaratibu wa magari kuingiza maji ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite kupitia matenki.
Kuhusu barabara amemuagiza Kaimu meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro Magaka Gishi kufuatilia changamoto hiyo kwa kufikisha kwa mtendaji mkuu ili lifanyiwe kazi.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika