Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Ikungi
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeweza kuwasaidia wakulima wa alizeti kwa kuhamasisha kila kaya kulima zao hilo kuanzia ekari moja hadi tatu, nia ikiwa kuwawezesha kiuchumi, kwani zao hilo soko lake ni kubwa ndani na nje ya nchi.
Lakini pia halmashauri hiyo imeweza kuwasaidia kupata mbegu za alizeti za ruzuku kwa sh. 5,000 kwa kilo moja badala ya sh. 20,000, hivyo kutoa nafuu kubwa kwa wakulima, huku wakiweza pia kuwasambazia mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwandishi wa makala haya, amefanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwenye Banda la Ikungi la Maonesho ya Nanenane ya kitaifa yaliyofanyika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 8, 2024.
Kijazi anasema halmashauri hiyo wakulima wake wanategemea kilimo kwa shughuli zao za kupata kipato kwa asilimia 80 hadi 85, huku halmashauri hiyo kwa Mapato ya Ndani inategemea wakulima kwa asilimia 65, hivyo ndiyo maana wameweka mkazo kuwaendeleza wakulima hao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kilimo bora.
“Katika kuhakikisha zao la alizeti ndiyo linakuwa zao kuu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, kwanza tumeweza kufanya uhamasishaji wa msimu wa kilimo kwa kuhakikisha kila kaya angalau inalima ekari moja hadi tatu za alizeti.
Lakini pamoja na hiyo, tumeweza kutoa elimu ya jinsi ya kulima alizeti kwa kutumia kanuni bora ya kilimo ambayo ndiyo itaweza kumtoa mkulima na kuweza kupata tija.
Na tatu, tuweza kutoa mbegu bora yenye ruzuku ya Serikali ambayo ingembidi mkulima ainunue kwa sh. 20,000 kwa kilo moja, lakini kwa kupitia ruzuku ameinunua kwa sh. 5,000 kwa kilo moja.
“Hiyo ndiyo Rais Dkt. Samia ameweza kutusaidia katika Sekta ya Kilimo, hasa katika zao la alizeti kwenye wilaya yetu na mkoa wetu wa Singida. Lakini pia, tumeweza kusambaza mbolea ya ruzuku kwenye vijiji vingi kati ya vijiji 101 vilivyopo ndani ya kata 28 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, ambapo asilimia 70 ya vijiji vilifikiwa na mbolea hiyo, ambapo tani 257 zimeweza kutumika kwenye wilaya yetu kwa msimu wa 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 88 ukilinganisha na msimu wa 2022/2023 ambao tulisambaza tani 36 tu” anasema Kijazi.
Kijazi anasema kwa kutumia mbegu ya ruzuku ambayo ilikuwa na ubora, na mbolea ya ruzuku, wakulima waliitikia na kuweza kulima kwa wingi na manufaa yake wameyaona.
Kijazi anasema halmashauri hiyo, pamoja na mazao mengine ambayo wanalima, inategemea mazao makuu matatu ambayo ni alizeti ambalo ni zao kuu la biashara, kuna mtama ambalo ni zao kuu la chakula, na mbogamboga yaani vitunguu ambalo pia ni zao kuu la biashara, na katika nanenane hiyo wamekwenda kuonesha zao la alizeti, mtama na vitunguu.
Na wameweza kulima alizeti hiyo iliyopandwa kwa mbegu ya kisasa kwenye Shamba Darasa. Pia wamepanda mtama na vitunguu.
“Kwenye Nanenane hii tumeweza kuonesha zao la alizeti ambalo ndiyo linampa mkulima fedha nyingi, na tumeonesha ukulima wa kisasa wa zao hili.
Tumeonesha unaweza kuwa na mbegu mbalimbali za alizeti, na zikaonesha mafanikio kutokana na mazingira yetu, na katika kipando hiki cha alizeti tuna mbegu aina nne ambazo ni Sunbloom ambayo ni mbegu yenye ruzuku ya Serikali, na tuliweza kuletewa na tumewasambazia wakulima wetu ambao wameweza kuzalisha.
“Lakini tuna mbegu ya pili aina ya Seedco LG, ambayo tumeweza kuionesha katika vipando hivi, na wakulima wamekuja kujifunza. Pia tuna mbegu ya Aguara 6 ambayo nayo ni mbegu chotara na inaweza kuhimili katika mazingira yetu, na nne ni Super Sun 66, nayo ni mbegu chotara ambayo ina uwezo wa kuzalisha mazao kwenye mazingira yetu. Hivyo katika maonesho haya ya nanenane, tumemuonesha mkulima namna anaweza kutumia mbegu hizo akapata manufaa” anasema Kijazi.
.
Kijazi anasema mkulima atakaetumia mbegu hizo za alizeti huku akifuata kanuni bora za kilimo atapata kati ya gunia 12 hadi 18 kwa ekari moja, na ataachana na kilimo cha mazoea ambacho kinampa gunia tatu hadi tano kwa ekari moja, na wakulima wengi wa Ikungi wameanza kubadilika, na wameanza kutumia mbegu bora, ambapo zamani walikuwa wanatumia nafaka, mazao waliyozalisha ndiyo wanafanya mbegu.
“Kwa kutumia mazao waliyolima kuwa mbegu, uzalishaji ulikuwa unadumaa mwaka hadi mwaka, lakini kwa sasa uzalishaji unaongezeka mwaka hadi mwaka, lakini kwa sasa uzaliahaji kwenye wilaya yetu umeongezeka kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Cha kwanza kabisa ni baada ya Serikali kuanza kutoa mbegu ya ruzuku, ambapo mwaka 2021/2022 tuliweza kupokea mbegu ya ruzuku tani 35, msimu wa 2022/2023 tulipokea mbegu ya ruzuku tani 77.
“Na uzalishaji wetu uliongezeka kutoka tani 26 hadi tani 74 kwa msimu huo wa 2922/2023, na sasa tupo kwenye mavuno kwa asilimia 70, na tuna mategemeo ya kuvuna mavuno tani 84 ya zao la alizeti, mpaka sasa hivi tunavyoongea, wakulima wameshavuna kwa asilimia 76 takribani tani 58, na wameanza kuuza na bei bado ni nzuri” anasema Kijazi.
***KILIMO CHA PAMBA
Wilaya ya Ikungi ina hali ya hewa nzuri inayofaa kwa kilimo cha Pamba. Kata zinazolima zao hilo zipo 11, ambazo ni Kikio, Misughaa, Siuyu, Mtunduru, Igombwe, Mwaru, Makilawa, Minyughe, Iglansoni, Mkiwa na Issuna.
***SKIMU ZA UMWAGILIAJI
Wilaya ya Ikungi ina skimu moja ya umwagiliaji katika kata ya Mangonyi, skimu hiyo ina ukubwa wa ekari 450. Kwa mwaka 2022/2023 skimu imeweza kuzalisha tani 84 za mahindi na mbogamboga.
***KILIMO CHA UMWAGILIAJI KANDO KANDO YA BONDE LA KIDEKA.
Baadhi ya wakulima mmoja mmoja au katika vikundi katika baadhi ya Kata za Puma, Kituntu, Ikungi, Mang`onyi,Mkiwa, Issuna, Dung`unyi,Mtunduru, Unyahati, Sepuka, Irisya na Mwaru, wanatumia pampu ndogo kumwagilia mashamba ya mbogamboga na miwa pamoja na mabwawa na mito ya asili.
***HALI YA CHAKULA
Hali ya chakula kwa kipindi hiki inaridhisha, kwani wakulima wengi ndio wanavuna mazao yao, na mavuno yako juu ya lengo la mkulima kwa kuwa hali ya unyeshaji wa mvua ilikuwa nzuri katika msimu wa 2023/2024. Halmashauri katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo hali ya chakula kwa halmashauri yao imekuwa nzuri na hakuna upungufu wa chakula kwa kuwa wakulima wamezalisha hadi kupata ziada kwa ajili ya biashara.
***MIKAKATI YA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA PAMBA
“Uzalishaji wa pamba umeimarishwa kutokana na hatua zifuatazo: Kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya kanuni 10 za kilimo bora cha pamba.
Kusimamia usambazaji, uuzaji na ukopeshaji wa pembejeo ya zao la Pamba. Kusimamia Sheria na Kanuni zinazohusu zao la pamba kwa kutochanganywa zao hilo na mazao mengine. Kuhakikisha Maafisa kilimo wa kata na vijiji wameandaa mipango kazi yao na kuisimamia.
“Maafisa kilimo wamepewa vitabu vya kutunzia kumbukumbu ili kunukuu shughuli zinazofanyika kila siku kwa kuainisha, jina la mkulima, huduma aliyopata, namba ya simu ya mkulima aliyehudumiwa na saini ya mkulima.
Pikipiki 28 zimegawanywa kwa Maafisa Ugani ngazi ya kata na vijiji. Pia kusimamia maelekezo ya Serikali kuwa zao la pamba liuzwe kwa mfumo wa Ushirika ili kumsaidia mkulima kupata bei nzuri ya zao husika na kuona tija ya uzalishaji wake” anasema Kijazi.
***HALI YA UKUSANYAJI NA UUZAJI WA PAMBA
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekusanya na kuuza pamba jumla ya kilo 844,639 zenye thamani ya sh.929,102,900. Kilo zilizosafirishwa ni 844,639 zenye thamani ya sh. 929,102,900. Kilo zilizolipwa ni 844,639 zenye thamani ya sh. 929,102,900.
Halmashauri imepata ushuru wa sh 27,873,089. Kwa msimu wa 2024/25 wameshakusanya jumla ya kilo 273,141 sawa na thamani ya sh. milioni 440, na mavuno yako katika asilimia 40.
***MIKAKATI YA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA ALIZETI
**Hali halisi ya uzalisha wa zao la alizeti, takwimu zinaonesha katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, zao la alizeti uzalishaji wake unaongezeka, na hiyo ni kutokana na jitihada mbalimbali ambazo wilaya iliona zinafaa kuchukuliwa.
Kwa msimu wa 2020/2021 ilikuwa tani 26,288, msimu wa 2021/2022 tani 46,283.7, msimu wa 2022/23 tani 74,413, na msimu wa 2023/24 ilikuwa tani 58,913, na mavuno bado yanaendelea yako katika asilimia 70 ya mavuno.
“Hapo awali uzalishaji ulikuwa mdogo sana kutokana na baadhi ya changamoto kama vile upatikanaji na matumizi duni ya mbegu bora, bei kubwa ya mbegu chotara, wakulima kutozingatia kanuni za kilimo bora, Mabadiliko ya Tabianchi ,Mfumo wa Masoko ya ununuzi wa alizeti usio rasmi, matumizi hafifu ya zana bora za kilimo hali iliyopelekea kutokidhi mahitaji ya viwanda 204 vilivyopo ndani ya mkoa (Singida) ambavyo vinahitaji jumla ya tani 623,055 kwa mwaka na Viwanda Vidogo 19 vinavyohitaji malighafi tani 208,050. Kutokana na changamoto hiyo, halmashauri ilichukua mkakati wa kuongeza uzalishaji kama ifuatavyo:-
“Kupanua/kuongeza eneo litakalolimwa zao la alizeti, uhamasishaji umefanyika kwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazao (Mkuu wa Wilaya) kwa kuhakikisha kuwa maeneo ya uzalishaji yanaongezaka na jumla ya ekari 112,230 kutoka kwa wakulima wapya. Kutenga maeneo mapya ya uwekezaji kwa ajili ya kilimo cha alizeti na jumla ekari 78,230 zimetengwa, na tayari ekari 53,200 zimeshapata wawekezaji.
Kuhakikisha mbegu bora zinapatikana na zinatumika ipasavyo Tuliweza kupokea mbegu zenye ruzuku ya serikali na Halmashauri ilihakikisha inasambaza mbegu hizo na zinalimwa, kuzalisha mbegu za kuazimiwa (QDS) kwa kupitia Vikundi, na jumla ya tani 10.2 za mbegu zilizalishwa, kushirikiana na wadau wa pembejeo ili kusogeza huduma kwa karibu” anasema Kijazi.
Kijazi anasema pia wametoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ya Ruzuku ya Serikali hasa katika zao la alizeti.
Kuimarisha upatikanaji wa zana bora za kilimo kwa kuwakaribisha wawekezaji wawekeze katika sekta ya zana za kilimo kama vile trekta, mashine za kupandia na kuvunia, kuimarisha huduma za ugani kuhakikisha kila afisa ugani anakuwa na shamba la mfano na mashamba darasa, na jumla ya mashamba darasa yapatao 96 kwa msimu wa 2023/24 yalikuwepo.
***KOROSHO
Kijazi anasema zao la korosho ni miongoni mwa mazao yanayolimwa katika halmashauri yao na, hiyo ni kutokana na utafiti uliofanyika kutoka TARI na Chuo Kikuu cha SUA kuwa zao la korosho linastawi katika ukanda wao wa Mkoa wa Singida na Kanda ya Kati. Takribani hekta 5,116 sawa na ekari 12,790, zimepandwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 katika mashamba ya mkulima mmoja mmoja na mashamba ya pamoja (Block farming) katika kijiji cha Mkiwa na Ulyapiti .Mavuno kwa sasa ni machache kutokana na changamoto mbalimbali
Ambapo, changamoto zinazokabili shughuli za uendelezaji wa zao la korosho ni pamoja na hali ya hewa (Mabadiliko ya Tabianchi) ikiwemo ukame na wadudu waharibifu.
Wakulima kutokua na teknolojia bora ya uzalishaji wa zao hilo, hali inayowalazimu wazalishe zao hilo kwa mazoea, hivyo kuathiri maendeleo yake. Bei ghali za pembejeo za zao hilo na upatikanaji wake ni mgumu.
***MIKAKATI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KOROSHO
Wakulima wameshauriwa kufanya usafi (palizi) kwa kupanda mazao mengine ya muda mfupi yatakayosaidia shamba kuwa safi kipindi chote pamoja na kupunguzia matawi (pruning) ili kuondoa masalia ya wadudu na magonjwa pamoja na kuyachoma moto masalia yote.
“Tumeanza kupokea Ruzuku ya Pembejeo ya viuatilifu kutoka Bodi ya Korosho, na kwa mwaka 2023/2024, tayari tumepokea lita 1,000 na zimeshasambazwa kwa wakulima.
Tumesambaza mbegu na miche ya mikorosho kwa msimu wa 2023/24 tumesambaza tani moja ya mbegu za korosho, kuweka ruzuku ya pembejeo, kwani itawahamasisha wakulima wengi kutumia pembejeo kila inapobidi, pamoja na kuwa karibu zaidi na wakulima wa mikoa inayoanza uzalishaji hasa katika kanda hii ya kati” anasema Kijazi.
Na kwa kuongeza, halmashauri hiyo imeratibu zoezi la upatikanaji wa mbegu za zao hilo kutoka Naliendele Mtwara kupitia Bodi ya Korosho, na mbegu hizo zitawasili hivi karibuni na zitasambazwa kwa wakulima. Pia Halmashauri kwa kushirikiana na Tree for the feature, wamezalisha miche 10,000 na wamezisambaza kwa wakulima. Lengo Ikiwa halmashauri kuongeza chanzo kipya cha mapato na mkulima kuwa na kipato endelevu kwakuwa zao hilo ni zao la kudumu.
***MIFUGO NA UVUVI
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ni moja ya halmashauri ambazo wananchi wake wanafaidika na uvuvi wa samaki, na kuweza kupata kipato kinachowasaidia kujiendeleza kimaisha.
Kwa wastani tani 960 za samaki zinavuliwa katika kata za Mgungira, Mwaru na Iyumbu. kupitia Bwawa la Wembere. Pia kuna ufugaji wa kutumia mabwawa ambapo wafugaji takribani 20 wanaendelezwa.
“Shughuli za uvuvi zinafanyika katika Bwawa la Wembere ambapo samaki wanaovuliwa ni perege, kambale na kamongo. Kwa mwaka wastani wa tani za samaki zinazovuliwa kwa mwaka ni 960 katika Kata za Mgungira, Mwaru na Iyumbu. Pia kuna ufugaji wa kutumia mabwawa, ambapo wafugaji takribani 20 wanaendelezwa. Pia tuna bwawa la Muyanji ambamo uvuvi wa kujikimu unafanyika” anasema Kijazi.
Kijazi anasema halmashauri hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 8,860 ambapo kati ya hizo, kilomita za mraba 3,737 zinafaa kwa ufugaji. Na aina na idadi ya mifugo ni ng’ombe wa asili 417,746, ng’ombe wa maziwa 6,512), mbuzi wa asili 221,355, nguruwe 843, kuku wa asili 913,773 na kuku wa kisasa 28,122.
Amezitaja faida zitokanazo na ufugaji na uvuvi kuwa ni chanzo cha lishe bora kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na maeneo mengine Tanzania. Chanzo cha kipato kwa wakulima na wavuvi, na chanzo cha Mapato ya Ndani ya Halmashauri na maduhuli ya Serikali Kuu
Anasema miundombinu ya mifugo iliyopo, wilaya ina jumla ya Majosho 38, kati ya hayo Majosho 16 yanafanya kazi, tisa yapo kwenye ukarabati na 13 ni mabovu kwa kiwango kikubwa. Mabanda ya ngozi yapo saba, minada mitano (Sepuka, Njiapanda, Mtavira, Kaugeri na Ilolo), vituo vya afya ya mifugo vinne (4) (Ikungi, Ihanja, Sepuka na Mungaa),
“Makaro ya kuchinjia tisa (Issuna, Njiapanda, Ihanja, Sepuka, Ikungi, Mungaa, Mgungira, Ighombwe na Puma), Malambo / mabwawa 35 ambayo yote ni mabovu na mbuga moja ya Wembere kama sehemu ya uvuvi, vibanio vya kudumu vya mifugo viwili (Mwaru na Mkiwa), na Mabirika ya kunyweshea maji mifugo 16” anasema Kijazi.
Anasema katika malengo ya kupunguza vifo vya mifugo, kupitia Sekta ya Mifugo, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikitoa huduma za mifugo katika msimu wa mwaka 2022/2023 na 2023/2024. Halmashauri imefanikiwa kukinga magonjwa ya mifugo kwa kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mapele Ngozi (Lumpy Skin) ngombe 49,628, Mbwa 7,832 dhidi ya Kichaa cha Mbwa (Rabies), kuku 518,703 dhidi ya ugonjwa wa Kideri (Newcastle), kuku 362,927 dhidi ya ugonjwa wa Gumboro na kuku 72,472 dhidi ya ugonjwa wa Ndui (Fowl pox),.
“Kuogesha mifugo kuzuia usambazaji wa magonjwa, ng’ombe 283,173, mbuzi 137,082, kondoo 89,361, mbwa 4,920, na nguruwe 6,284 wameogeshwa na madawa yakuua wadudu wanaokaa kwenye ngozi za mifugo, Mifugo kupewa dawa za minyoo, ambapo ng’ombe 238,073, mbuzi 109,836, kondoo 47,261, kuku 579,362, mbwa 5,973 na nguruwe 4,284 wamenyeshwa dawa za minyoo, na kutoa huduma ya matibabu imetolewa kwa mifugo iliyopata magonjwa na kupona kwa asilimia 97” anasema Kijazi.
Kijazi anasema kwenye Sekta ya Uvuvi, Wilaya ya Ikungi ina jumla ya Mialo mitatu kwa ajili ya shughuli za uvunaji samaki kukiwa na wavuvi wapatao 507, Mitumbwi 198 na kuna ofisi tatu za usimamizi wa rasimali za uvuvi ambazo ni ofisi za wataalamu wa mifugo wa kata husika kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji, kata na halmashauri.
“Wastani wa mavuno kwa mwezi ni tani 80 ambazo hutofautiana kulingana na majira, wakati wa mvua uzalishaji unakua juu ukilinganisha na kiangazi ambapo sehemu kubwa ya Bwawa hukauka. Pia tuna wafugaji wadogo wa samaki kwa njia ya mabwawa takribani wafugaji 20 ambao wanaendelea kupatiwa elimu ya ufugaji wa kisasa kwani bado wanafuga kienyeji na upatikanaji wa mbegu bora za vifaranga wa samaki.
Shughuli za uvuvi pia hufanyika katika Bwawa dogo la Muyanji linalopatikana katika kata ya Makiungu na Mungaa japokua uzalishaji wake bado ni mdogo” anasema Kijazi
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika