June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia alivyorejesha tabasamu yawastaafu, TUCTA, wabunge wafunguka

Na Joyce Damiano, TimesMajira Online

JUNI 13, 2024 na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 alitangaza mabadiliko ya kikokotoo yaliyoshusha kundi la wafanyakazi waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50 mpaka asilimia 33 na kundi waliokuwa wakipokea asilimia 25 walipandishwa mpaka asilimia 33

Dkt. Mwigulu alisema Rais Samia ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliopo sasa hadi asilimia 40. Hilo ndilo kundi kubwa la watumishi wanaofanya kazi nzuri sana kwa taifa letu wakiwepo, walimu, kada ya afya, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na makundi mengine yalioko Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Aidha, Waziri Mwigulu Rais ameelekeza kuongezewa zaidi kundi lililokuwa likipokea asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33 sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka wa fedha huu.

“Hii inadhihirisha kuwa Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anawapenda sana Watanzania, hivyo basi na sisi Watanzania Tusimame na MAMA kwa kumpatia wasaidizi makini kutoka Chama Cha Mapinduzi watakaoendeleza gurudumu la maendeleo kupitia uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.

Akizungumza Bungeni juzi  Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi, anasema 17,068 waliostaafu kazi kuanzia Julai mwaka 2022 watalipwa mapunjo yao ya mafao ya mkupuo kulingana na kikokotoo kilichotangazwa  Juni 13,2024 na Waziri Mwigulu.

Akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 alisema;

“Suala la kikotoo linaonesha ni namna gani Rais Samia anawajali wafanyakazi wake.

Julai 2022 kuna mabadiliko yawekwa kuhusu kikokotoo, ambapo watumishi wa umma walitoka kulipwa asilimia 50 wakaenda 33 na wale waliokuwa asilimia 25 walipanda kwenda asilimia 33,” anasema.

Anasema jambo hilo lilikuwa ni kilio kikubwa kwa wafanyakazi ambao mishahara yao ya chini na wengine husubiria mkupuo wa fedha hizi kuanza maisha yao pale wanapoona kuwa wamestaafu.

Anasema Rais Samia kama alivyosikia kilio cha madaraja, kilio cha madeni na aliagiza kikotoo kiweze kuangaliwa na kwamba baada ya Waziri wa Fedha kukaa na ofisi yake waliangalia namna nzuri zaidi ya kutatua changamoto hiyo kwa kutenga sh. bilioni 155 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.

Anasema wamesikia kilio cha wabunge na vyama vya wafanyakazi kunyanyua kiwango hicho kwenda pale kilipokuwa, lakini kadri ya utengamavu wa mifuko ya jamii inavyoendelea na kila uhimilifu unavyofanyika Serikali itaendelea kuangalia ni namna gani inarejea katika asilimia 50.

“Hao wanaokwenda kulipwa si wale wanaokwenda kustaafu Julai mwaka 2024, wanakwenda kulipwa wote hata wale waliostaafu Julai 2022,”alisema.

Anasema wastaafu 17,068 waliostaafu kuanzia Julai 2022, wanakwenda kulipwa mapunjo yao ya asilimia saba na wale waliokuwa wakipata asilimia 33 watalipwa mapunjo yao ya asilimia mbili.

Ndejembi anasema wanatarajia kuona wengi wakienda kudai mapunjo ya mafao yao ya mkupuo.  Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alisema kwa kuwa wastaafu hao hao waliopunjwa wanafahamika, Serikali iwalipe bila kusubiri waende kudai.

“Nafikiri hiyo ni lugha tu ya mazungumzo, lakini walipeni tu la sivyo maombi yatakuwa ni mengi sana,” anasema.

Kufuatia usikivu huo wa Rais Samia,  Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, anaipongeza Serikali kwa kuja na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi malalamiko ya wafanyakazi ambayo yamekuwepo kuhusu Kikokotoo cha awali.

Aidha, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) wameishauri Serikali kuangalia upya na kuweka usawa katika nyongeza ya mkupuo ya kikokotoo kwa watumishi ambao wameguswa na mabadiliko haya ya Sheria ya Watumishi wa Umma.

Ikumbukwe kwamba kabla ya mabadiliko hayo, TUCTA kwa nyakati tofauti ilipeleka maombi kwa Rais Samia kufanyia mabadiliko kikokotoo hicho, ambapo ilisema Mstaafu anapokuwa ombaomba kwenye nchi aliyoijenga mwenyewe, sio jambo zuri.

 Ilikuwa ikisema kwamba Serikali kuwalipa wastaafu kiasi hicho ni kukosa shukurani kwa waliolitumikia Taifa kwa miaka mingi.

“Kwa kuwa mifuko inaonesha kuimarika Serikali ione haja ya kuboresha kanuni hizo bila kuathiri mifuko hiyo,” alisema Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Mkunda alipohutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei 1, mwaka huu.  

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya anapongeza uamuzi huo wa Serikali, akisema; “Sasa rai yangu wamesema wamefikisha asilimia 40 na wamesema kuwa wataongezea kwa kipindi cha muda mfupi hadi watakapoona kuwa iko sawa.

“Kikubwa ninachoweza kusema nipongeze kwa hiyo hatua lakini kiukweli bado kwa sababu kabla ya sheria kubadilishwa ilikuwa ni asilimia 50,” anasema Bulaya.

 Anataka kilio cha wafanyakazi kiendelee kufanyiwa kazi ili wanapomaliza utumishi wao basi wapate kitu wanachostahili. “Nchi nyingine zinaondoka na asilimia 60 hadi asilimia 70, kwa hiyo sisi mifuko yetu kuwa hoehae na iliyosababisha ni Serikali yenyewe.

Kisiwe kigezo cha kuwaminya wale wanaokatwa kila mwezi ili mwisho wa siku wapate mafao yao yatakayoweza kuwaandalia maisha mazuri ya kustaafu,” anasema.

Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, mbali na kupongeza anasema alitamani wastaafu wagepewa kiasi chote cha asilimia 50 kama ilivyokuwa awali.

Hata hivvyo, anasema kiasi cha asilimia 40 ambacho Serikali imekitoa ni hatua kubwa na anaona Serikali imefanya vizuri kwao.

“Mbunge wa Nkenge, Florent Kyombo anasema Rais Samia, amepunguza makali yaliyokuwa kwa wastaafu kwa kubadilisha kikokotoo.

Anamshukuru Rais kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi na kwamba anaamini hata mapokeo kwa wastaafu walioko mitaani watakuwa wamepokea kwa moyo wa shukrani kwa kuwa Rais Samia amesikia kilio chao.

Kwa upande wao wasomi, wanaharakati na wananchi wanasema ongezeko la kikokotoo litaongeza morali ya kazi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Dkt. Damian Sambuo, anasema uamuzi wa Serikali kusikiliza kilio cha wastaafu kuhusu malipo ya mkupuo ya kiinua mgongo utarejesha upya matumaini ya Watanzania katika uwajibikaji.

Anasema hatua hiyo inaleta mwanga mpya kwa watumishi wa umma na sekta binafsi. Ni kete kwa serikali kujenga morali ya watumishi wake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Dar es Salaam, Padri Dkt. Francis Ngatingwa, anasema mwelekeo wa bajeti ya 2024/25, ni mzuri, lakini kuna shida anayoona ya kutegemea mikopo kutoka nje.