January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia alivyopambana na ubambikiaji kesi 2022

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar

TANGU Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amekuwa akionya tabia ya wananchi kubambikizwa kesi.

Amekuwa akiwataka Polisi na ofisi za masuala ya sheria kuhakikisha vitendo vya ubambikizaji kesi vinakoma na mashauri yanayofikishwa mahakamani yanakuwa na ushahidi wa kutosha.

Kati ya mambo ambayo amesisitiza kwa mwaka huu 2022 na pamoja na kutaka washtakiwa wanapokamatwa kuwe na ushahidi ili kesi zao zisikilizwa na kumalizika kwa wakati ili haki itendeke mapema.

Tangu atoe maelekezo hayo tumeona mabadiliko makubwa katika sekta hiyo, kwani washtakiwa wengi waliokuwa wakisotoka gerezani kwa takribani miaka mitano kwa kesi za ufisadi na uhujumu uchumi zimefutwa.

Uamuzi huo wa Rais Samia umerejesha furaha kwenye familia nyingi ambazo wapendwa wao walikuwa wakisota gerezani kwa miaka mingi, kesi zao zikitajwa na kuahirishwa kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.

Miongoni mwa walionufaika na maelekezo hayo ni pamoja na James Rugemalira, ambaye baada ya kuachiwa breki yake ya kwanza ilikuwa ni Kanisani kwa ajili ya kushukuru Mungu kwa kuachiwa.

Nyuma ya Rugemalira wapo washtakiwa wengi walioachiwa kufuatia agizo hilo la Rais Samia. Kwa uamuzi huo tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Samia, maana mwaka 2022 ameutumia kuwafuta machozi washtakiwa wengi waliokuwa na kesi ambazo zilikuwa zikipigwa kalenda kwa ushahidi kutokamilika.

Kundi lingine ambalo limenufaika na msimamo huo wa Rais Samia, ni washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na kesi zenye mwelekeo wa kisiasa, na hiyo ilitokana na mazungumzo maridhiano baina ya CHADEMA na Serikali. Mazungumzo hayo yaliasisiwa na Rais Samia na Mbowe.

Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu alikaririwa akimshukuru Rais Samia akithibitisha kuachiwa kwa wafuasi wa chama hicho.

Aidha, huko nyuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahi kuonya vitendo hivyo wakati wa uzinduzi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mkoani Dodoma.

Alisema nimatarajio ya Serikali kuwa kila moja ya ofisi hizo itapanua wigo wa utendaji wake hadi kufikia ngazi ya wilaya.

“Ofisi hizi zinategemewa kuwa mkono wa Serikali katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji kesi vinakoma na kuhakikisha kuwa kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi wa kutosha,” alinukuliwa akisema Waziri Mkuu.

Alisema malengo makubwa ni kuufanya umma kuelewa vizuri masuala ya kisheria na utoaji haki, ikiwa pamoja na kufanya mabadiliko yenye tija kwa sheria.

“Na mabadiliko hayo yaanze kwanza na sheria zetu kusomeka kwa lugha ya Taifa, lakini pili uendeshaji kesi nao uangaliwe, uoaji hukumu nao uangaliwe na hata hati za hukumu nazo zisomeke kwa lugha ya kiswahili ili watu wakawaida waweze kuwa na uelewa mpana katika suala hili,” alisema.

Kauli viongozi hao ilikuja wakati muafaka ambapo kuna baadhi ya malalamiko ndani ya jamii yakilaumu baadhi ya vyombo mbalimbali vya haki ikiwepo ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali kwa kushindwa kutekelza wajibu wake ipasavyo na hivyo watu wengi kujikuta wakiwekwa mahabusu muda mrefu kutokana na kile kinachoelezwa upelelezi wa kesi zao kutokamilika.

Tabia hii imefanya watuhumiwa wengi kujikuta wakitumikia adhabu kwa kukaa mahabusu muda mrefu na wengine miaka kadhaa kwa madai tu kwamba upelelezi wa kesi zao haujakamilika.

Haya ni mambo ya msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi sambamba na kauli ya Waziri Mkuu kuagiza kukomeshwa kwa vitendo vya ubakizaji kesi kwa wanachi wengi wasio na hatia.

Leo hii ndani ya magereza zetu watu wengi wanatumikia adhabu kwa makosa ya kubambikwa yasiyo na msingi. Hata ndani ya mahabusu zetu kuna watuhumiwa wengi wamewekwa na wengine chuki tu za kubabikwa makosa ambapo kama waendesha mashitaka watazingatia ushauri wa Waziri mkuu watu hao hawawezi kukaa hata siku moja mahabusu.

Lipo tatizo lingine la msingi kabisa katika uzembe huu ambapo baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wale wanaotuhumiwa kufilisi na kuangusha vyama mbalimbali vya ushirika kujikuta wakisota rumande muda mrefu na wengine kufikishwa mahakamani bila kuwepo upelelezi wa kina wa kufanyaa kesi zao zianze kusikilizwa.

Ni jambo la aibu pale baadhi ya watuhumiwa wanaposombwa kwa jazba na kuswekwa rumande bila kufanyika upelelezi wa kina na mwisho wa siku kuonekana upelelezi ni dhaifu na kuachiwa na mahakama.

Yapo matatizo mengi yanayotajwa na kulalamikiwa na wananchi kwamba yamekuwa kero kubwa katika tasnia ya usimamizi wa haki hapa nchini. Hali imesababisha baadhi ya watuhumiwa kuona jambo hili kuwa na misukumo ya mikono ya itikadi za siasa katika baadhi ya mashauri.

Kwa mtazamo na maelezo ya wananchi baadhi ya watu wanajikuta wakiumia na kukosa haki kwa mitazamo fulani ya kiitikadi.

Lazima ieleweke kwamba ni dhambi kubwa kwa vyombo vya haki kupora haki ya mtu ama kuweka mashinikizo yenye harufu za kiitikadi.

Ofisi za masuala ya sheria zina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji kesi kuanzia Polisi vinakoma na mashauri yanayofikishwa mahakamani yanakuwa na ushahidi wa kutosha wa kufanya kesi hizo kuanza kusikilizwa.

Ni aibu kubwa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani kwa ushahidi dhaifu matokeo yake ni upande wa Jamhuri kuaibika kwa kupoteza kesi husika na wakati mwingine watuhumiwa kukata rufaa na kudai fidia ya mamlilioni ya kutokana tu na uzembe wa upelelezi.

Nasema hivyo kutokana na kile kinachoonekana kwamba uchunguzi wa baadhi ya kesi kwenye maeneo mengine zikiwemo zile za vyama vya ushirika huko nyuma, zilionesha kuchukua sura za kiitikadi na kuacha kabisa ile dhana ya taaluma na maadili (Ethics & Professionalism) kwenye kufanya uchunguzi na kutenda haki sawa kwa watuhumiwa wote.

Mbali na kuwaumiza watuhumiwa udhaifu huu pia unaweza kutafsiriwa kuwa ni namna fulani ya baadhi ya watendaji wachafu kutengeneza mazingira ya kuwaumiza wananchi kesi ili kulazimika kupata fedha kwa njia zisizo halali.