May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aleta neema kwa wakulima wa Tumbaku Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MIAKA miwili ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani imeleta neema kubwa kwa wakulima wa zao la tumbaku Mkoani Tabora baada ya Makampuni yaliyopewa dhamana kununua tumbaku yote inayolimwa na wakulima.

Wakulima wameeleza kufurahishwa na hatua ya Makampuni hayo kutoweka kikwazo cha kununua kwa makisio ya awali pekee kama ilivyokuwa huko nyuma, hali ambayo imeongeza hamasa kwa wakulima wengi zaidi kulima zao hilo.

Wakiongea na mwandishi wa gazeti hili kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji cha Msange, Kata ya Kalunde katika halmashauri ya manispaa Tabora wamesema kuwa zao hilo sasa ni kimbilio la wakulima kutokana na manufaa wanayopata.

Mkazi wa Kijiji hicho Subira Salumu ambaye ni mkulima na Katibu (Meneja) wa Chama Cha Msingi Twende Pamoja ameeleza kuwa awali chama chao kilikuwa na wakulima 25 lakini sasa wameongezeka hadi kufikia 392 ndani ya miaka 2.

Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka 2 kilimo cha tumbaku kimeleta tija kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho na vijiji vingine baada ya kutatuliwa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu ikiwemo kucheleweshwa pembejeo.

‘Msimu uliopita tulikisia kuzalisha kilo 500,000 lakini tukazalisha kilo 520,000 na zote zikanunuliwa na Kampuni ya Alliance One, baada ya kuuza tulipata zaidi ya sh bil 2.4, na kila mkulima alipata fedha zake taslimu pasipo kukopwa’, amesema.

Mwenyekiti wa Chama hicho Ramadhan Mohamed ameishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kujali wakulima na kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo na masoko, sasa hivi hakuna usumbufu tena, kiasi chochote kinachozalishwa kinanunuliwa.

Ameongeza kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali ya Rais Samia katika sekta ya kilimo yamewezesha wakulima wa zao hilo katika kijiji hicho na maeneo mengine kupata manufaa makubwa ikiwemo kujenga nyumba za kisasa, kununua vyombo vya usafiri na kusomesha watoto wao.

Chiku Rajabu mkulima mkazi wa Kata ya Kalunde katika manispaa hiyo amesema kuwa tangu aanze kulima zao hilo zaidi ya miaka 10 iliyopita walikuwa hawana masoko ya uhakika na walikuwa wanapewa ukomo wa kilo za kuzalisha lakini sasa hakuna ukomo.

‘Tunamshukuru sana mama yetu Rais Samia kwa kutuletea wanunuzi wa kutosha na ruzuku ya mbolea, sasa hivi tunauza bei nzuri, mwaka jana nililima ekari 4 nikavuna kilo 5600 ambapo nilipata zaidi ya sh mil 23, si haba’, amesema.

Alitoa wito kwa wanawake wenzake kuchangamkia fursa za kilimo hasa kilimo cha zao hilo ili kujikwamua kiuchumi, na kusisitiza kuwa kilimo kinalipa wasikae nyumbani na kusubiri kuletewa kila kitu na waume zao.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kalunde Sizya Kagoma amempongeza Rais Samia kwa kusikia kero ya wakulima na kuwaondolea vikwazo vilivyokuwa vikiwarudisha nyuma kiuchumi, sasa wanafurahia serikali yao.

Ameshauri makampuni yote yaliyopewa dhamana ya kununua tumbaku ya wakulima katika Mkoa huo kuhakikisha yanajipanga vizuri katika kipindi hiki cha msimu wa mavumo ili masoko yatakapoanza kila mkulima apate stahiki yake.

Naye Afisa Ugani wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU) Michael Zakaria amesema kuwa hadi sasa jumla ya makampuni 7 yameruhusiwa na serikali kununua zao hilo Mkoani hapa.

Ametaja baadhi ya makampuni hayo kuwa ni Alliance One, Japan Tobacco International (JTI), Mkwawa Tobacco Leaf, Vodi cel, Magefa, TLTC na nyinginezo.