Na Raphael Okello, TimesmajiraonlineBunda
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa mkono wa pole na rambirambi kiasi cha sh. milioni 80 kwa waathirika wa ajali ya gari katika Kijiji cha Kyandege wilayani Bunda mkoani Mara.
Akiwasilisha kwa waathirika hao jana salaam hizo za rambirambi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Vicent Naano aliwaambia waathirika hao kuwa Rais amepokea taarifa za ajali kwa masikitiko makubwa, hivyo ametoa rambirambi na kifuta machozi kiasi cha sh. milionini 80.
Alisema familia ambazo ndugu zao wamepoteza maisha watapokea kiasi cha sh. milioni 5 kwa kila familia na wale waliopata majeraha watoto kwa wakubwa watapokea kiasi cha sh. milioni 1.4.
Naano alieleza kuwa wao kama Serikali wilayani Bunda watazidisha juhudi za kukagua magari ili ajali kama hizo zisijirudie.
Wakipokea rambirambi hizo, familia zilizoathirika walitoa shukrani kwa Samia huku zikieleza kuwa wao kama raia ni mara ya kwanza kwao wilayani Bunda kupewa rambirambi na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Ajali hiyo iliyoua watu 9 na kujeruhi takariban watu 18 ilitokea Agosti 25 mwaka huu ambapo gari aina ya Hiace waliokuwa wakisafiria kutoka wilayani Serengeti kwenda Bunda ilipata ajali katika kijiji cha Kiandege wilayani Bunda, chanzo kikielezwa kuwa ni kupasuka kwa tairi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase, alisema jeshi la Polisi bado linamsaka dereva wa gari hilo , Emmanuel Matoto aliyetokomea kusikojulikana baada ya ajali hiyo na kwamba mmiliki wa gari hilo ni Sospiter Kamoga Maila.
Aliwataja wanaume walifariki dunia ni Giney Manywea, Benjamini Nyamagege na Mateo Ngetengwa. Kwa upande wa wanawake ni Mkami Romore, Kyora Makuru, Anna Mashalla, Rahel Molemi na Nyaishi Tongoshe ambapo mtu mmoja jina lilikuwa halijapatikana.
Aidha majeruhi ni 18, ambapo kati yao wanaume ni 13 na wanawake ni watano. Kamanda Morcase alisema majeruhi hao wengine wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya DDH wilayani Bunda na wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya DDH -Bunda na kwamba imeshatambuliwa na ndugu zao na taratibu za kuchukua miili hiyo kwa mazishi zinaendelea.
Ajali mbalimbali kwa wiki hii imeikumba baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara ambapo mwanzoni mwa wiki hii watoto sita ambao ni wanafunzi kutoka kijiji cha Ochuna wilayani Rorya walipoteza maisha baada ya kunasa kwenye tope walipokuwa wakiogelea.
More Stories
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto
Jela miezi sita kwa kuvaa sare za JWTZ
Watolewa hofu uvumi juu ya uwepo wa Teleza