*Asema limeendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake, lampa matumaini makubwa kwamba kesho ya nchi yetu na watoto, ni salama, asisitiza halina mpango wa kuwa jeshi la uvamizi
Na Penina Malundo,Timesmajiraonline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kwa miaka 60 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa jeshi hodari katika utekelezaji wa majuku yake na limekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wakati wa majanga, ambapo limeendelea kuwa jeshi la ulinzi na sio la uvamizi na halina mpango huo.
Rais Samia alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati wa akifunga Maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi hilo sherehe zilizofanyika katika Uwanja vya Uhuru, zikitanguliwa na maonesho ya kijeshi pamoja na zana za kivita.
Kiongozi huyo ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama bchini, alisema katika kipindi chote cha miaka 60 yote Jeshi hilo halijawahi kuvamia nchi yoyote na wala halina mpango huo.
Alisema kihistoria jeshi hilo halikujengwa katika misingi ya kuwa jeshi la uvamizi, bali jeshi la Wananchi hivyo litaendelea kulinda amani ya nchi na kuhimiza nchi majirani kudumisha amani kwenye nchi zao.
Kwa mujibu wa Rais Samia pamoja na amani iliyopo nchini, Jeshi linaendelea kujiimarisha katika nyanja zote kwendana na misingi ya kuundwa kwake, dhamira yao ni kujenga Jeshi imara ambalo lipo tayari kwa hali zote na wakati wowote.
”Mimi binafsi kama Amri Jeshi Mkuu kila ninapotembelea au kushiriki shughuli za Jeshi letu, nashuhudia utayari, uhodari na umahiri, lakini ujasiri wa Jeshi hili, naridhika kuwa Jeshi letu lipo katika kiwango cha juu na kunipata matumaini makubwa kwamba kesho ya nchi yetu na watoto wetu ipo salama,” alisema Rais Samia.
Alisisitiza kwamba Jeshi hilo litaendelea kuwa jeshi la kisasa lenye dhana na nyenzo la kisasa, hivyo waendelee kufanyakazi wakijua Amiri Jeshi Muu yupo nao wakati wote.
“Tunaimarisha Jeshi liende na mabadiliko ya kiteknolojia ya vifaa na dhana, mikakati na mbinu za medani ili kuwezesha kutimiza wajibu wake ipasavyo,” alisema Rais Samia. Alisema Jeshi la Tanzania limekuwa ni la ukombozi na kioo katika harakati za ukombozi wa Afrika na kulinda amani Duniani.
”Katika ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kila raia anawajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha Uhuru, mamlaka ardhi na umoja wa kitaifa, hivyo katika mafanikio ya Jeshi letu, wananchi wa Tanzania wana mchango wao,” alisema Rais Samia na kuongeza;
”Sote tunakumbuka wakati wa Vita ya Kagera namna wananchi walivyojitolea kwa hali na mali kuliunga mkono Jeshi letu, kwani wananchi wamekuwa msingi wa ulinzi wa amani wa nchi yetu na umoja wetu ndani ya taifa.”
Rais Samia alisema kupitia kilele cha maadhimisho hayo anawasihi wananchi wa Tanzania kuendelee kutimiza wajibu wao wa Kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza kulinda amani ya nchi, huku wakiwakataa na kukemea wanaochochea uhasama na uvunjifu wa amani ndani ya nchi.
”Katika Kipindi cha miaka 60 Jeshi limekuwa ni kimbilio la wananchi na kuwa mstari wa mbele kutoa misaada ya huduma pale wananchi wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo majanga ya asili au ajali.
”Wananchi wanakumbuka mchango wa jeshi katika uokozi nchi ilipopatwa na mafuriko ya Kilosa na Ulanga mwaka 1970, ajali za kuzama Meli Mv Bukoba na Meli ya Mv Spice Bahari ya Zanzibar mwaka 2011 na hivi karibuni mwaka 2024, Janga la maporomoko ya udongo Hanang’a pamoja na kutoa huduma hizi ndani ya nchi pia jeshi limetoa huduma hizi nchini Malawi mwaka 2023 walipopatwa na majanga ya maporomoko kama yalitupata Tanzania,”alisema alisema
Alisema Jeshi limekuwa kinara katika kutafsiri dira,sera na mipango ya Serikali katika awamu zote za uongozi ambapo kwa awamu ya kwanza ya uongozi tTaifa la Tanzania lilitangaza vita kuwa ni maadui watatu, yaani Ujinga,Maladhi na Umaskini, ambapo katika kupambana na adui ujinga Jeshi lilianzisha shule kadhaa katika ngazi tofauti, kuelimisha watu, katika adui maladhi napo wanatoa huduma za afya na ni huduma za kutegemewa, huku kwa upande wa adui umasikini Jeshi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linawapa vijana hali na stadi za kazi ili waweze kujiajiri na kupambana na umasikini wa kipato.
Rais Samia alisema hivi karibuni Jeshi limetekeleza kwa vitendo miito yote inayotolewa na Serikali ikiwemo katika kushiriki kwenye ujenzi wa IKulu mpya ya Chamwino Dodoma,Ujenzi wa ukuta wa Mererani wenye urefu wa kilomita 24.5 kama moja ya jitihada ya kulinda rasilimali madini inayovunwa katika eneo hilo.
Alisema katika kutekeleza kauli mbiu ya kazi iendelee, Jeshi linajitekeleza katika mageuzi yaendanayo katika mifumo ya ulinzi na uchumi duniani.
”Nchi yetu ina mkakati wa taifa wa kuimarisha uchumi na upatikanaji wa fedha za kigeni, malengo makuu ni kuimarisha uzalishaji wa mauzo ya bidhaa na huduma, kuzalisha bidhaa na huduma mbadala zinazoagizwa kutoka nje na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji binafsi ndani na nje ya nchi,”alisema.
Alisema kazi ya kuuwisha na kuimarisha viwanda vyake ili viweze kuzalisha baadhi ya mahitaji yake nchini na kunusuru matumizi ya fedha za kigeni.
Akizungumzia suala la nidhamu na utiifu, Rais Samia alisema katika Jeshi hilo ameshuhudia askari ambao wanaenda kinyume na misingi mikuu Jeshini wakichukuliwa hatua bila ya kuchelewa.
Rais Samia alisema utiifu wa Jeshi letu nchini,ndio unaojenga imani kwa Watanzania kulithamani na kuliamini na kuwa na matarajio makubwa ya jeshi lao. ”Niwasihi Makamanda na wapiganaji hakikisheni imani hiyo mnailinda kwa nguvu kubwa sana,”alisisitiza Rais Samia.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito