December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aiongezea MSD mtaji wa bilioni 100/-

Na Reubenkagaruki, TimesmajiraonlineDodoma

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa kiasi cha sh. bilioni 100 kama mtaji wa kuwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya.

Mbali na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, fedha hizo zitasaidia kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dodoma waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MSD katika Kanda ya Iringa na Kanda ya Dodoma.

Tukai alisema fedha hizi zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kuweza kutengeneza mikakati itakayofanya taasisi iweze kununua kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali.

Aidha, alisema Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24, bidhaa za afya zenye thamani ya sh. bilioni 22.1 zilinunuliwa kutoka kiasi cha sh. bilioni 14.1 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57.

“Dhamira hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kuvutia wawekezaji ambapo matumizi ya fedha za kigeni yatapungua na ajira zitatengenezwa nchini,” alisema.

Akieleza kuhusu Ushirikishaji wa Sekta Binafsi Katika kufanikisha adhma ya Serikali ya kushirikisha sekta binafsi, alisema MSD imetambua maeneo yanayohitaji ushirikiano na sekta binafsi na inafanya uchambuzi ili wawekezaji wenye sifa waweze kushiriki kwenye uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya.

Aidha, alisema MSD imekua ikifanya mawasiliano na balozi zetu zikiwemo Balozi za China, Korea Kusini, Urusi, Algeria na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu kwa wazalishaji wa ndani.

Kuhusu uanzishaji wa Viwanda vya Kuzalisha Bidhaa za Afya nchini, Tukai alisema Bohari ya Dawa ina viwanda viwili, ambavyo ni kiwanda cha barakoa kilichopo eneo la Keko, Dar es Salaam na kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi, mkoa wa Njombe.

Alisema Kiwanda cha Kutengeza Barakoa, Keko Dar es Salaam
Kiwanda cha kutengeneza Barakoa kinazalisha barakoa za kawaida na barakoa maalum (N95).

Alisema Barakoa hizi hutumika kwenye matumizi mbalimbali ya kawaida kwa lengo la kujikinga na maambukizi au vihatarishi vinginevyo na pia hutumiwa na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma nchini.

“Kiwanda cha barakoa kimefanikiwa kuzalisha na kusambaza barakoa zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 4 na kufanya nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa barakoa,” alisema.

Kwa upande wa kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono (Gloves) kinapatikana eneo la Idofi- mkoa wa Njombe na kimeanza uzalishaji mwezi Februari 2024.

Alisema hadi kufikia Juni 2024, Kiwanda kimeweza kuzalisha jumla ya gloves zaidi ya milioni 4.

“Hadi sasa, kiwanda hiki kimetoa ajira zipatazo 136 kwa wakazi wa eneo la Makambako na kufanya ununuzi kwenye kampuni mbalimbali ziliozopo eneo la Makambako.

Kwa kutengeneza mipira ya mikono ya kiuchunguzi “examination gloves” pekee kiwanda kitaweza kuokoa zaidi ya sh. bilioni 11,” alisema.