*Ni wakati akihutubia mkutano wa FOCAC, asema licha ya changamoto zilizoukabili uchumi wa Dunia imeendelea kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mikutano mbalimbali
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline China
RAIS. Samia Suluhu Hassan, amesema licha ya changamoto zilizoukabili uchumi wa dunia kwa miaka ya hivi karibuni, Serikali ya China imeendelea kuwa rafiki wa kweli kwa kuhakikisha utekelezaji wa kiwango cha ju cha makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano
mbalimbali ya Jukwaa la Ushirikiano.
Rais Samia ameyasema hayo jana wakati wa funguzi wa Mkutano wa FOCAC uliofanyika katika ukumbi wa the Great Hall of the People.
Akihutubia katika mkutano huo, Rais Dkt. Samia amesema Mkutano wa FOCAC wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa kuwa unafanyika muongo mmoja kamili baada ya kupitishwa na kuzinduliwa kwa Mkakati wa Afrika na China uliozinduliwa jijini Dar es Salaam na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake ya kwanza barani Afrika mwaka
2013.
Rais Samia alisema matokeo ya ushirikiano imara na madhubuti kati ya China na Afrika yanadhihirika kupitia maendeleo makubwa ambayo nchi nyingi za Afrika wameyapata kupitia ushirikiano wa nchi hizo na China.
Aidha, ushirikiano baina ya China na Afrika umekuwa chachu katika kukuza chumi za nchi nyingi za Afrika pamoja na kuleta mendeleo ya watu kupitia miundombinu na ukuaji wa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo na vikubwa.
Akihutubia wakati akifungua Mkutano huo, Rais Xi Jinping alisema China iko tayari kushirikiana na Afrika katika maeneo anuwai ikiwa ni pamoja na kufuta kodi kwa bidhaa zinazotoka nchi za Afrika ambazo tayari zina uhusiano na China.
Aidha, Rais Xi alisema mahusiano ya China na nchi za Afrika utazingatia vipaumbele vya mendeleo ili kuhakikisha uchumi jumuishi wa pande hizo mbili.
Ahadi nyingine alizozitoa Rais Xi ni pamoja na utayari wa China kuunga mkono nchi ambazo zitakazokuwa wenyeji wa Mashindano ya Youth Olympics ya mwaka 2026 na mashindano Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027.
Hali kadhalika, Rais Xi alisema China itawekeza kwenye masuala ya afya, ikiwemo ujenzi wa viwanda vya dawa pamoja na kutoa uzoefu katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alishiriki Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa ambapo amesema liicha ya ajenda ya kilimo kuwa ya muda mrefu barani Afrika, inakosa ukuaji wenye tija, hivyo bara hilo linahitaji kuungwa mkono na nchi zilizoendelea kama China ili kunufaika na kilimo cha kisasa.
Rais Samia amesema Tanzania imeendelea kuweka mkazo katika kuendeleza
sekta ya kilimo na viwanda, na ilieleza jitihada za Serikali ya kuhakikisha michango wa vijana katika kilimo unakuwa kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT) ambayo imelenga kuwafanya vijana kushiriki katika kilimo chenye tija.
Hata hivyo, Rais Dkt. Samia amesema jitihada za Serikali pekee hazitoshi, hivyo amewaalika sekta binafsi kuja chini kuwekeza kwenye mbegu bora, vifaa, vya kisasa
vya kilimo pamoja na ujenzi wa skimu za umwagiliaji ili kuweza kulima kilimo cha kisasa na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa kilimo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito