December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ahimiza wakulima nchini kulima kilimo cha kisasa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameagiza wakulima nchini kuanza kulima kilimo cha kisasa cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akieleza yaliyojiri katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Tanzania uliofanyika hivi karibuni nchini China.

Waziri Silinde alisema kauli hiyo ya Rais inahusu mkakati wa kukuza kilimo cha kisasa, ambapo wizara ya kilimo imepewa jukumu la kujenga mabwawa na kuvuna maji ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinafanikiwa.

“Hii ndiyo kauli mbiu yetu sasa, kama tulivyoelekezwa na Rais, kuhakikisha tunajenga mabwawa na kutumia maji kwa kilimo badala ya kutegemea mvua pekee,” alisema Silinde.

Akifafanua zaidi, Silinde alisema kuwa China imetenga kiasi cha dola bilioni 360 kwa Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Sehemu ya fedha hizi itaelekezwa moja kwa moja kwenye sekta ya umwagiliaji nchini Tanzania, ambapo mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima.

Aidha, Silinde alieleza kuwa katika kipindi hicho, Serikali itahakikisha miradi yote ya umwagiliaji iliyopo inakamilishwa na miradi mipya itaanzishwa ili kuwasaidia wakulima kote nchini.

“Tumejipanga kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilishwa na miradi mipya inaanzishwa ili kuwasaidia wakulima wetu kufikia malengo,” aliongeza.

Silinde pia alibainisha kuwa mkutano huo umefungua milango kwa Tanzania kuuza bidhaa zake za kilimo nchini China, ambapo awali hakukuwa na ruhusa hiyo. “Tumepata fursa ya kuuza bidhaa zetu za kilimo nchini China. Tayari tumesaini makubaliano ya kuuza mashudu na pilipili,” alisema.

Aliongeza kuwa, wakati wa ziara hiyo, Serikali pia ilisaini mkataba na Mainland Group, kampuni inayojenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mafuta ya alizeti nchini Tanzania. Kiwanda hicho kinatarajiwa kusaidia kukidhi mahitaji makubwa ya mafuta ya alizeti nchini, na hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.