*Yaichapa Guinea 2-1
Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa shilingi milioni 500, iwapo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, itafuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), itakayofanyika nchini Morocco.
Akitoa ahadi hiyo jana kwa niaba ya Rais, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma aliwatia moyo Taifa Stars huku akiwapa salamu kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iwapo watafuzu michuano hiyo.
“Tukifuzu kwenda AFCON 2025 ya Morocco kuna shilingi milioni 500 mezani,” alisema Mwinjuma akitoa salamu za Rais Samia kwenda kwa wachezaji wa Taifa Stars.
Taifa Stars ilifanikiwa kuondoka na alama tatu baada ya kuibuka na ushindi ugenini wa goli 2-1 katika mchezo wa pili wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025, dhidi ya Guinea.
Mchezo huo wa Kundi H, ulichezwa jana kwenye dimba la Charles Konan Banny, Yamoussoukro nchini Ivory Coast, licha ya wenyeji kuonekana kuutawala mchezo.
Katika mchezo huo Milango ilikuwa migumu mpaka mapumziko kutokana na safu ya ulinzi ya timu zote kuonekana kuwa imara.
Kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko huku kila mmoja akihitaji ushindi ili aweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu michuano hiyo.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa timu ya Taifa Stars, ambapo dakika 61 Feisal Salum aliachia mkwaju mkali nje ya 18 na kuifungia timu yake goli la kwanza huku goli la pili likitiwa kimiani na Mudathir Yahaya dakika ya 89.
Goli la kufutia machozi kwa timu ya Taifa ya Guinea, lilifungwa na Mohamed Bayo dakika ya 57 baada ya kumzungusha beki wa Stars Ibrahim Abdallah ‘Bacca’.
More Stories
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship
Mnzava apania kuwapeleka vijana Simba na Yanga