November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi abainisha maeneo matano umuhimu uchumi wa bluu

  • TEF yaipongeza NSSF kwa kutoa msamaha wa tozo kwa waajiri wa sekta binafsi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) huku akibainisha maeneo matano muhimu kuhusu uchumi wa bluu ambao ndio sera na mwelekeo wa Serikali anayoiongoza.

Akifungua mkutano huo katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil mjini Zanzibar, Dkt. Mwinyi alisema uchumi wa bluu una sekta tano kubwa ikiwemo utalii, uvuvi na ufugaji wa samaki, bandari, usafiri na biashara za baharini pamoja na mafuta na gesi.

Rais Dkt. Mwinyi alisema hayo ndio maeneo muhimu katika kukuza na kuendeleza uchumi wa buluu ambapo alitumia fursa hiyo kulipongeza jukwaa la wahariri kwa uamuzi wake wa kuamua kufanya mkutano huo visiwani Zanzibar wenye kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Buluu na Mawasiliano ya Umma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil mjini Unguja. Mara baada ya kuhutubia Mhe. Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi alifungua rasmi mkutano huo. Mkutano huo umedhamiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo NSSF ambayo ilipata fursa ya kutoa semina kwa wahariri kuhusu hifadhi ya jamii, majukumu na Utendaji wa Mfuko

Awali, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alizishukuru taasisi za Serikali ikiwemo NSSF kwa kuwaunga mkono katika mkutano huo.

Balile alisema NSSF inafanya mambo mengi mazuri hasa katika kuunga mkono juhudi mbalimbali za wadau pamoja na kutatua changamoto za wanachama ambapo Bodi ya Wadhamini ya Mfuko ilitoa msamaha wa tozo kwa waajiri waliokuwa na malimbikizo ya michango kwa muda wa miezi mitatu na kufanikiwa kukusanya zaidi ya sh. Bilioni 39 katika kipindi hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, uliozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kupitia mkutano huo NSSF ni mdhamini mkuu.

Naye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema uamuzi wa jukwaa la wahariri kufanya mkutano wake Zanzibar ni ushahidi tosha kuwa Rais Dkt. Mwinyi anafanya kazi nzuri na kwamba wamekuja kuunga mkono mawazo ya Serikali yake ya kuifanya Zanzibar kuwa njema kupitia uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita alisema iko haja kwa wahariri kujifunza zaidi ili wanapotoa taarifa ziendane na zile sera za Serikali hasa kueleza maendeleo ya uchumi wa bluu.