January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi: Barabara Pemba zitajengwa kwa lami

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia Wananchi wa Pemba kuwa Barabara nyingi Kisiwani humo zitajengwa kwa Kiwango cha Lami.

Rais Sk, Mwinyi ametoa tamko hilo alipozindua Barabara za Kilomita 10 za Micheweni – Kiuyu-Maziwa Ng’ombe na Barabara ya Michweni -Shumba Mjini hadi Bandarini Wilaya ya Micheweni ,Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Aidha amefahamisha kuwa Serikali Ina Programu Maalum ya Kuziwekea Taa Barabara zote zilizojengwa kwa Kiwango cha Lami nchi nzima.

” Hatuwezi Kujenga Barabara kiwango cha lami halafu taa zitushinde” alisema Dk, Mwinyi

Amesisitiza kuwa Barabara zilizofikia Ujenzi wa Kuwekwa Kifusi zikiwa Barabara kuu au Zile za ndani zote zitawekwa lami.

Rais Dk , Mwinyi amewahimiza Wananchi kuacha kujenga katika Hifadhi za Barabara kwani zimetengwa maalum kwa ajili ya kuendeleza Miundombinu mengine.

Dk, Mwinyi ameeleza kuwa kumekuwa na Tabia ya Watu kujenga Pembezoni mwa Barabara kwa kutegemea kulipwa Fidia na Serikali jambo ambalo sio sahihi.

Rais Dk, Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa Nyumba zilizokwepwa na Barabara ziondoshwe na kuacha wazi hifadhi ya Barabara.

Rais Dk, Mwinyi amezitaka Halmashauri Kusimamia suala hilo na kudhibiti Utoaji wa vibali holela vya Ujenzi Pembezoni mwa Barabara.

Akizungumzia bei za Chakula Dk, Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeamua Kuzijenga Bandari za Mkoani ,Shumba Mjini na Mkoani ili bidhaa zinazotoka nchi za nje ziweze kupelekwa Moja kwa moja Pemba hatua itakayopunguza gharama za Usafirishaji .

Rais Dk,Mwinyi amesisitiza kuwa itamkabidhi Mkandarasi aliejenga Bandari ya Mkoani Bandari za Shumba Mjini na Wete ili aanze Ujenzi Hivi karibuni ili kufikia Lengo hilo.

Aidha Rais Dk, Mwinyi amewathibitishia Wananchi kuwa Serikali itaikabidhi Kampuni IRIS iliojenga Barabara zilizozinduliwa za Micheweni kazi ya kuziunganisha na Barabara kuu barabara ndogondogo ziliyomo Micheweni.

Akiwasilisha Taarifa ya Kitaalamu ya Ujenzi wa Barabara Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Dk, Habiba Hassan amesema Ujenzi wa Barabara hizo zenye Urefu wa Kilomita 10 ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 ,Dira ya Maendeleo ya Zanzibar, Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Taifa na Mpango Mkuu wa Usafiri ambapo Barabara zenye Urefu wa Kilomita 140.9 zimejengwa Unguja na Kilomita 134.9 zimejengwa Pemba.