May 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi aipongeza Kampuni ya Yas kushirikiana na ZHC

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Kampuni ya Mawasiliano ya Yas kwa kushirikiana na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), kurahisisha malipo ya huduma za makazi.

Pongezi hizo alizitoa hivi karibuni Visiwani Zanzibar, wakati wa hafla ya uzinduzi wa ZHC Connect App, mfumo mpya wa kidijitali uliolenga kurahisisha malipo ya huduma za makazi kupitia Shirika la Nyumba.

Rais Mwinyi amesema, ushirikiano huo
utafungua ukurasa mpya wa utoaji huduma kwa njia za kidijitali, hatua ambayo italeta urahisi, uwazi, na ufanisi kwa wananchi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, (wa pili kutoka kushoto), akikabidhi cheti cha shukrani kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha (wa pili kutoka kulia) kama ishara ya kutambua mchango wa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas katika kushirikiana na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), katika fupi iliyofanyika hivi karibuni Visiwani Zanzibar, Kushoto ni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali na kulia Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mixx nya Yas, Angelica Pasha amemshukuru Rais Mwinyi kwa kukubali kuungana nao katika tukio hilo muhimu.

Lakini pia, kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuijenga Zanzibar mpya na ya kisasa.

Pasha amesema, wao Kama Yas by Mixx wamefurahi kuona hatua kubwa ya maendeleo kwa uzinduzi wa toleo jipya la ZHC Connect App, mfumo ulioboreshwa mahsusi kwa usimamizi wa malipo mbalimbali ya Shirika la Nyumba Zanzibar, sambamba na uzinduzi rasmi wa mradi wa Mwinyi Housing Scheme.

“Mixx by Yas, tunajivunia kuwa sehemu ya mageuzi haya muhimu yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya teknolojia jumuishi na rafiki kwa mtumiaji.

“Mkakati wetu kama Mixx by Yas ni kuhakikisha kuwa huduma zetu zinapatikana kwa urahisi, kwa usalama, na kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kila Mtanzania, wakiwemo wakazi wa Zanzibar.

“Kupitia ushirikiano wetu na Shirika la Nyumba Zanzibar, tumefanikisha kuunganisha mfumo wa ZHC Connect na huduma za Mixx by Yas, hivyo kuwawezesha wananchi na wateja wa ZHC kufanya malipo ya huduma zote kwa njia ya kidijitali bila kutoka nje ya mfumo,” amesema Pasha.

Amesema, kwa sasa wateja wanaweza kufanya malipo ya kodi, ada za vibali, kuhuisha mikataba, na kuwasilisha maombi ya nyumba moja kwa moja kupitia simu zao kwa kutumia control number ya Serikali – kwa usalama, kwa haraka, na kwa uwazi.

Aidha, amesema wanaamini kuwa teknolojia inapaswa kusaidia pia taasisi za umma kuongeza uwajibikaji, uwazi, na ufanisi – mambo ambayo ni muhimu sana katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo amesema, mafanikio ya teknolojia hayawezi kufikiwa bila elimu ya kutosha kwa watumiaji wake.

Kwa kutambua hilo, wametoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya mfumo huo kupitia kampeni za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na kupitia mitandao yao ya kijamii, ili kila mwananchi aweze kunufaika kikamilifu na huduma hizo.

Vilevile, amesema Kampuni ya Yas, inajivunia pia kushirikiana katika mradi wa Mwinyi Housing Scheme, mradi wenye lengo la kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kumiliki makazi yao kwa njia rahisi na ya kidijitali.

“Kupitia ZHC Connect na Mixx by Yas, wananchi wataweza kuwasilisha maombi na kufanya malipo ya nyumba kwa urahisi bila kulazimika kufika ofisi za ZHC.

“Tumejipanga pia kuiunganisha ZHC Connect moja kwa moja ndani ya Super App ya Mixx by Yas ili kuongeza urahisi na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za Shirika la Nyumba,” amesema..

Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa serikali walihudhuria wakiwemo, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Viongozi wa Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi.