May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mstaafu Dkt. Kikwete, Afisa Mtendaji mkuu wa GPE wakoshwa na utekelezaji mradi

Na Mwandishi Maalumu, TimesMajira Online, DSM

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bibi Laura Frigenti, leo wametembelea na kukagua shule za Msingi ya Maji Matitu iliyoko Mbagala na Mikongeni iliyoko Gongo la Mboto jijini Dar es salaam.

Katika ziara hiyo, iliyofanyika siku tatu kabla ya mkutano wa Bodi ya GPE utakaofanyika Zanzibar kuanzia mapema wiki ijayo, wamejionea shule ambazo Shirika hilo lImefadhili miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Madarasa, Vyoo na Mafunzo endelevu ya Walimu kazini na kueleza kuridhishwa na utekelezaji.

Katika shule ya Maji Matitu shirika hilo limefadhili ujenzi wa madarasa nane na matundu 20 ya vyoo, wakati katika shule ya Mikongeni imechangia ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo.

Akiongea baada ya ziara hiyo, Dkt. Kikwete ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na GPE katika kuboresha sekta ya elimu hususan elimu kwa wasichana na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi na mikakati ya kuiendeleza sekta hiyo.

Dkt. Kikwete, ambaye ni Mwafrika wa kwanza kuongoza GPE, amesema shirika hilo hadi sasa limeishaipatia Tanzania jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 332 (takriban shilingi 834,980,332,000.00) ili kusaidia sekta ya elimu bara na visiwani.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE Bibi Frigenti ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya Elimu katika nchi zenye uhitaji, akisisitiza kwamba changamoto nyingi za kimaisha zinaweza kuepukika endapo wananchi watapatiwa elimu bora.

Bi. Frigenti ameeleza kuridhishwa na matumizi ya Fedha ambayo GPE imekuwa ikitoa kwa Tanzania na kuahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na uliodumu kwa miaka 10 sasa.

Bi Fringeti ameisifia serikali kwa kuendelea na juhudi zake za kuendeleza elimu kwa kujenga miundo mbinu bora na kuhakikisha kila mtoto anapatiwa haki ya elimu na kwa kuweza kufanya mageuzi makubwa ya elimu .

Katika ziara hiyo Viongozi hao waliambatana na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deo Ndejembi. Naibu Katibu Mkuu WyEST Dkt Franklin Rwezimula.

Kwa niaba ya Serikali Viongozi hao wameishukuru GPE kwa kufadhili miradi ya elimu na kipekee kumshukuru Mhe. Kikwete kwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutafuta rasilimali za kuimarisha Sekta ya Elimu.

November 30, 2023 GPE imetiliana saini na Serikali ya makubaliano ya kutoa dola za Kimarekani milioni 85 (takriban shilingi 210) kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu.

GPE iliyoanzishwa mwaka wa 2002, ni Shirika linalosimamiwa na Benki ya Dunia, ambalo linajumuisha washirika mbalimbali wa maendeleo katika elimu.