WASHINGTON, Serikali ya Marekani imesema inasikitika kwamba raia nchini Jamhuri ya Kiisalamu ya Iran hawakuweza kushiriki katika uchaguzi huru na haki wakati wa uchaguzi wa rais nchini humo.
Hiyo ni kauli ya ya kwanza kutoka Marekani kuhusiana na ushindi wa mhubiri Ebrahim Raisi mwenye msimamo mkali wa kidini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema kuwa, raia wa nchi hiyo walinyimwa haki ya kuwachagua viongozi wao katika mchakato huru wa uchaguzi.
Wakati huo huo, hisia mseto zinaendelea kutolewa kuhusu ushindi huo wa Raisi huku Israel ikisema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuwa na wasiwasi kutokana na ushindi wake kwa sababu ya kujitolea kwake kuendeleza haraka mpango wa kijeshi wa nyuklia.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Lior Haiat alisema kuwa, kuchaguliwa kwa Raisi kunaweka wazi nia mbaya ya Iran na jamii ya kimataifa inapaswa kuwa na wasiwasi.
Raia wengi wa Iran walisusia kura hiyo baada ya wagombea wengi kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho na kusalia na wawaniaji saba pekee.
Kiongozi huyo wa kidini na mhafidhina mwenye msimamo mkali, Ebrahim Raisi alitangazwa Juni 19, 2021 kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais, katika matokeo yaliotarajiwa na wengi baada ya wagombea wengi wenye ushawishi kuzuiwa kuwania.
Maafisa wa uchaguzi walisema Raisi alishinda asilimia 62 ya kura baada ya kuhesabiwa takribani asilimia 90 ya kura kutoka uchaguzi wa Ijumaa.
Ushindi huo ulikuja bila hata kutangaza takwimu kuhusu kiwango cha ushiriki wa wapiga kura, baada ya wagombea wengine watatu kukubali kushindwa.
“Nawapongeza watu kwa chaguo lao,” amesema Rais anayemaliza muda wake Hassan Rouhani, ambaye amehudumu mihula miwili mfululizo na ataondoka madarakani mwezi Agosti, mwaka huu.
Raisi mwenye umri wa miaka 60 anachukuwa madaraka katika wakati huu ambao unatajwa kuwa muhimu ambapo Iran inatafuta kuokoa makubaliano yaliosambaratika ya nyuklia iliyofikia na mataifa makubwa na kujitoa katika vikwazo vikali vya Marekani ambavyo vimesababisha kuporomoka vibaya kwa uchumi wake.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja